Tuesday, June 21, 2011

MBIO ZA USHIRIKI KATIKA OLYMPIC ZAFIKIA PATAMU.

AFRICA
HATIMAYE mbio za kuwania nafasi tatu za ushiriki wa michuano ya Olympic ya mwaka 2012 kwa mataifa ya bara la Afrika zimefikia patamu, baada ya kusalia kwa mataifa manane ambayo yanaingia kwenye michuano nane bora.

Mataifa hayo manane yamefahamika baada ya michezo iliyochezwa mwishoni mwa juma lililopita ambapo ukanda wa kaskazini na magharibi mwa bara la Afrika umetoa timu nyingi huku Afrika kusini ikipata nafasi pakee ya kuwasilisha kusini mwa bara hilo.

Mataifa kutoka ukanda wa kaskazini yaliyofanikiwa kupenya ni Morocco, Algeria pamoja na Misri huku mataifa ya ukanda wa magharibi yakiwa ni Senegal, Ivory Coast pamoja na Mali.

Morocco wametinga katika hatua hiyo baada ya kupata matokeo ya jumla ya mabao matatu kwa mawili ambapo katika mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita timu hiyo kutoka kaskazini mwa bara la Afrika ililazimisha sare ya bao moja kwa moja dhidi ya timu ya taifa ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Algeria wanasonga mbele kwa jumala ya mabao 3-2 dhidi ya , Zambia ambao walipata ushindi wa mabao mawili kwa sifuri wakiwa nyumbani, huku wakishindwa kulipiza kisasi cha kufungwa mabao matatu kwa sifuri katika mchezo wa kwanza.

Afrika Kusini wameitupa nje Benin kwa jumla ya mabao 6-4 ambapo katika mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita vijana wa Jacob Zuma walichomoza na ushindi wa mabao matano kwa moja, ambao umekuja baada ya kusago cha mabao matatu kwa moja walichokipokea katika mchezo wa kwanza waliocheza ugenini.

Timu ya taifa ya Misri, imeifunga timu ya taifa ya Sudan bao moja kwa sifuri, ambalo linaifanya nchi hiyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao mawili kwa sifuri ambapo katika mchezo wa kwanza Sudan walikubali kupachikwa bao moja kwa sifuri.

Ivory Coast wameiondoa Congo Brazzaville kwa jumla ya mabao matatu kwa moja ambapo katika mchezo wa kwanza taifa hilo la Afrika ya Magharibi lilipata ushindi wa mabao mawili kwa moja.

Nigeria wamesonga mbele kwa jumla ya mabao matatu kwa moja dhidi ya Tanzania ambao jana wamekubali kichapo cha mabao matatu kwa sifuri kabla ya ushidni wa bao moja kwa sifuri walioupata katika mchezo wa kwanza.

Hatua ya nane bora imepangwa kuanza December 02-18 mjini Dakar nchini Senegal ambapo mshindi wa kwanza hadi wa tatu watashiriki moja kwa moja kwenye michuano ya Olympic ya mwaka 2012 itakayofanyika jijini London nchini Uingereza na mshindi wan ne atapambana na mshiriki kutoka barani Asia.

No comments:

Post a Comment