Friday, August 27, 2010
*Kikosi cha Stars kitakachaivaa Algeria hiki hapa.
KIKOSI cha wachezaji 20 cha timu ya soka ya taifa, Taifa Satrs kitakachoivaa Algeria, kimetangazwa jana na Kocha mkuu wa timu hiyo Jan Poulsen.
Akizugumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa Habari za Michezo kwenye ukumbi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema uteuzi wa kikosi chake umezingatia umuhimu wa kila mchezaji kulingana na ugumu wa mechi hiyo.
Alisema mechi hiyo ya kwanza ya kinyang'anyiro cha kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika 2012, imepangwa kuchezwa Septemba 3, mwaka huu mjini Algiers, Algeria.
"Niliita kambini wachezaji 26 ili kujiunga na kambi ya Stars,lakini hata hivyo ni wachezaji 20 tu ambao wanahitajika kusafiri kwa ajili ya mecho huo. Hivyo kutokana na ukweli huo imenilazimu kuwaaacha baadhi ya wachezaji kutokana na kuwa majeruhi na wengine nafasi zao zimechukuliwa na wachezaji wa kulipwa," alisema.
Poulsen ambaye anakinoa kikosi hicho baada ya kumrithi kocha aliyetangaulia raia wa Brazil, Marcio Maximo aliwataja wachezaji waliochwa na klabu wanazotoka katika mabano ni kipa mahiri nchini, Juma Kaseja (Simba).
"Kipa Kaseja kama inavyofahamika ni majeruhi , na amefungwa POP. Daktari amempa wiki moja nyingine ili ajitazamie, hivyo ni bahati mbaya kwake naye ni miongoni mwa wachezaji sita watakaoikosa safari hiyo," alisema.
Wengine ni beki wa kushoto,Juma Jabu (Simba), viungo Athuman Idd 'Chuji' (Yanga) na Abdulhalim Humoud (Simba) na mshambuliaji Uhuru Seleman (Simba) na Jerson Tegete (Yanga).
Poulsen aliwataja wachezaji wanaondoka na kikosi hicho Jumanne ijayo na klabu wanazotoka katika mabano ni makipa Shaaban Kado(Mtibwa Sugar) na Jackson Chove (Azam FC).
Mabeki ni Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub'Cananavaro' na Stephano Mwasika (Yanga),Salum Kanoni na Kelvin Yondan (Simba), Aggrey Morris (Azam FC) na Erasto Nyoni (Azam FC).
Aliwataja viungo ni Jabir Aziz (Simba), Seleman Kassim(Azam FC), Nurdin Bakari (Yanga),Idrisa Rajabu (Sofapaka, Kenya) na Henry Joseph (Norway).
Wakati washambuliaji ni Danny Mrwanda (Dt Long, Vietnam), Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada), Abdi Kassim 'Babi' (Yanga), Mrisho Ngasa (Azam FC), Mussa Hassan 'Mgosi' (Simba) na John Bocco (Azam FC).
Akizungumzia mchezo huo, Poulsen alisema anatarajia kukutana na ushindani mkubwa kutoka kwa timu ya Algeria, kwani alisema hiyo inatokana na ukweli timu hiyo inaundwa na wachezaji wazuri na wana histori nzuri kwenye michuano mbalimbali barani Afrika.
Alisema lakini katika siku chache Stars ilizokaa kambini kujiandaa kwa pambano hilo, alisema amezifanyia kazi baadhi ya kasoro ndogo ambazo zilijitokeza kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars ambayo ilichezwa Agosti 11, mwaka kwenye Uwanja wa Taifa na ilimalizika kwa sare ya bao 1 - 1.
"Pamoja na kurekebisha dosari chache ambazo zilionekana kwenye mechi yetu dhidi ya Harambee, lakini ninatarajia kukutana na ushindani mkubwa kutoka kwa Algeria.Hiyo inatokana na ubora walionao wapinzani wetu, ila tutajitahidi tucheze vizuri ili hatimaye tushinde," alisema.
Naye Nahodha wa Stars, Nsajigwa akizungumzia mchezo huo, alisema wamejiandaa vizuri licha ya kuwa wanatarajia kukutana na ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani ambao watakua wakicheza kwenye uwanja wa nyumbani.
"Tumejiandaa vizuri kwa muda wote tuliokua kambini na Watanzania wana kila sababu ya kuiamini timu yetu, kwani licha ya kuwa mechi itakua ngumu lakini wanatakiwa kutuombea ili tuweze kuibuka na ushindi,"alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment