CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimesema kimeandaa tuzo maalum kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Pinto alisema tuzo hiyo imeasisiwa na uongozi mpya wa TASWA na ina lengo la kumpongeza na kumshukuru Rais Kikwete kutokana na mchango wake katika michezo na burudani.
Alisema katika muhula wake wa kwanza wa miaka mitano, alisema Rais Kikwete amekua mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa medani za michezo zinaboreka.
Pinto alisema ili kuona hilo linawezekana aliaamua kuwaleta nchini makocha wa soka, riadha na ngumi za ridhaa kutoka nje ya nchi ili kuona michezo hiyo inakua na kufika kiwango cha kimataifa.
Alisema mchakato wa kufanyika kwa hafla ya kumkabidhi tuzo kiongozi huyo, unaendelea na mara utakapomalizika utawekwa bayana ukumbi na siku chama chake kitakapotoa tuzo hiyo itakayotolewa nchini kwa mara ya kwanza.
“Kwa kweli TASWA hatuwezi kufumbia macho jitihada za masudi ambazo zimefanywa na Rais Kikwete kwenye muda wake huu wa miaka mitano, hivyo ili kuenze jitihada zake uongozi wetu mpya ulioingia madarakani Agosti 15, mwaka huu umepanga kumpa tuzo maalum,”alisema.
Aliwataja baadhi ya makocha ambao wako nchini na wanalipwa na serikali ya awamu ya nne ni, pamoja na kocha aliyemaliza mkataba wake Marcio Maximo alioyekua akiinoa timu wa Taifa Stars.
Wengine ni kocha wa ngumi za ridhaa raia wa Cuba, Giovanis Pimentel na makocha wengine wawili wa mchezo wa riadha ambao wote wanaendelea na kazi za kuzinoa timu za taifa za michezo husika.
Pinto alisema uongozi wake pia umepania kuongeza wigo wa semina mbalimbali kwa waandishi wa habari za michezo, alisema lengo la semina hizo ni kuongeza upea na ufahamu kwa wahusika.
Alisema uongozi wake pia umebadili mfumo wa uteuzi wa wanasoka bora wa kila mwezi, badala yake alisema TASWA itafanya uteuzi wa mwanasoka bora, mwandishi bora na mpiga picha bora wa mwaka.
“Tumefikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa uongozi wetu umeingia madarakani, huku kukiwa kumepita miezi takriban saba bila ya kuteuliwa kwa wachezaji bora wa mwezi. Hivyo ili kuepukana na usumbufu wa kuteua wachezaji hao, uongozi umeona ni vema kama utawateua wahusika baada ya kumalizika mwaka, alisema.
Alisema tuzo za mwandishi bora, mpiga picha na mtangazaji bora zimepangwa kufanyika Februari, mwakani ambapo tukio hilo alisema litariushwa ‘Live’ na televisheni.
Wakati huo huo, Pinto alisema TASWA imeandaa semina kwa waandishi wa habari za michezo ambayo itafanyika Septemba 18 na 19, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Alisema kimsingi semina hiyo itatoa mafunzo kuhusiana na michezo ya soka, riadha, mpira wa kikapu, tenesi na gofu.
“Nadhani hiyo itakua ni semina ya mwisho kwa mkoa wa Dar es Salaam msimu huu, kwani semina zingine zitakua zikifanywa mikoani kulingana na kanda zitakazopangwa na chama. Hatua hiyo inalengo la kupanua wigo wa uelewa wa uandishi habari za michezo nchini,” alisema.
No comments:
Post a Comment