Tuesday, September 7, 2010

BAADA YA VAN PERSIE, WENGER APATA PIGO LINGINE.

WINGA machachari wa timu ya Arsenal Theo Walcott atakuwa nje ya uwanja baada ya kupata maumivu ya kifundo cha mguu wakati timu yake ya Taifa ya Uingereza ikiibuka kidedea kwa kuifunga Switzerland mabao 3-1 katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Ulaya (Euro 2012).


Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alitolewa nje na machela baada ya Yves Oehri kumkwatua wakati akijaribu kumtengenezea Wayne Rooney nafasi ambayo ilizaa bao la kuongoza katika dakika ya 10.

Alichukuliwa moja kwa moja na kupelekwa hospitali katika jiji Basle kwa ajili kupigwa picha ya X - ray katika kifundo cha mguu wake wa kulia.

Kocha wa Uingereza Fabio Capello alifafanua kuwa maumivu aliyopata mchezaji huyo sio makubwa sana lakini hakuwa na uhakika na tatizo lenyewe.

Huu ulikuwa ni mchezo wa tatu kwa mchezaji huyo kuichezea timu hiyo toka alipoachwa katika kikosi kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini.

Walcott alianza vizuri mchezo katika mchezo kabla ya kuumia sekunde Rooney alipofunga bao la kuongoza akiamalizia krosi safi ya beki wa kulia wa timu ya Liverpool Glen Johnson.

Adam Johnson ambaye aliingia akichukua nafsi ya Walcott aliifungia timu hiyo bao la pili kabla ya Xherdan Shaqiri kufunga bao kwa shuti la mbali na kuipa matumaini timu yake.

Darren Bent ambaye nae pia aliingia kipindi cha pili ndio alipigilia msumari wa mwisho katika jeneza la wapinzani wao na kuendeleza rekodi ya ushindi ambapo Ijumaa iliyopita waliichabanga Bulgaria mabao 4-0 katika Uwanja wa Wembley.

Kuumia kwa Walcott kutakuwa ni mshtuko mkubwa kwa Kocha wa Arsenal, Arsen Wenger ambapo atakuwa akisubiri kwa hamu majibu ya mchezaji huyo baada kupungukiwa na washambuliaji wake.

Mapema Jumanne Wenger alipata taarifa za mshambuliaji Mdutch Robin van Persie ambaye atakuwa nje ya uwanja mpaka katikati ya mwezi Octoba akiuguza maumivu ya kifundo cha mguu.

Mshambuliaji mwingine wa Arsenal Nicklas Bendtner naye yuko nje ya uwanja akiuguza maumivu ya nyonga, wakati winga wake Samir Nasri natarajiwa kuanza mazoezi siku chache zijazo baada ya kuwa nje ya uwanja toka Agosti mwaka huu akiguza maumivu ya mguu.

No comments:

Post a Comment