Monday, November 15, 2010

"MNAMTWISHA MZIGO MKUBWA TEVEZ," - MANCINI

LONDON, England
KWA mara ya kwanza kocha wa Manchester City, Roberto Mancini, amesema nahodha, Carlos Tevez anabebweshwa mzigo mzito ndani ya kikosi hicho kulinganisha na wachezaji wengine Eastland.

Kocha huyo alimtolea mfano mshambuliaji mwenye miaka 23, Adam Johnson kuongeza kasi baada ya kinda huyo kushindwa kutamba katika mchezo dhidi ya Birmingham licha ya kucheza dakika 90 akichukuwa nafasi ya Tevez.

Mancini alisema, Johnson alishindwa kufunga mabao licha ya kupata nafasi nzuri na alionya Man City itapata ushindi wa kubahatisha ikiwa itamtegemea zaidi Tevez. Mtaliano alisema, Johnson na wachezaji wengine wa timu hiyo wanatakiwa kumsaidia Tevez kufunga mabao na siyo kubweteka.

"Adam Johnson siyo kiungo mkabaji, David Silva siyo kiungo wote ni washambuliaji. Lakini wana wana matatizo tangu kuanza msimu huu, ikiwa carlos hatafunga hakuna mchezaji yeyote anayeweza kufumania nyavu," alisema Mancini.

Mbali ya nyota, hao Man City ilimsajili mshambuliaji chipukizi wa Inter Milan, Mario Balotelli (20) aliyekuwa nje ya uwanja muda mrefu baada ya kufanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu. Man City ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 22 katika msimamo wa ligi.

Kocha huyo amekuwa akipata presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo na wachezaji wakikosoa mbinu zake za ufundishaji. Licha ya kumpa kitambaa cha unahodha Tevez, Mancini anapata shinikizo kwa wadau wa soka wanamtuhumu kutumia mabilioni ya fedha kusajili wachezaji nyota duniani lakini hapati mafanikio.

Mbali ya Balotelli na Silva, baadhi ya nyota waliotumia Eastland msimu huu ni kiungo wa Barcelona, Yaya Toure ambaye ni mdogo wa beki nguli na nahodha wa timu hiyo, Kolo Toure.

No comments:

Post a Comment