Monday, November 15, 2010

BLANC AKIPONDA KIKOSI CHAKE.

PARIS, Ufaransa
KOCHA wa Ufaransa, Laurent Blanc, amesema ni ndoto kwa timu hiyo kufanya maajabu katika mchezo wa soka duniani kwa kuwa kikosi hicho hakina wachezaji mahiri kama zamani.

Badala yake beki huyo wa zamani wa Manchester United alizitaka klabu za Ufaransa kuibua vipaji vipya kutoka mtaani. Blanc, alisema Ufaransa imepoteza mwelekeo baada ya wachezaji wake nguli kustaafu soka na haikuwa na msingi imara baada ya nyota hao kutundika daluga.

Blanc aliyechukua mikoba ya Roy Domenech, alionya Ufaransa inaweza kupoteza dira katika mchezo huo endapo hazitafanyika jitihada za kuibua wachezaji chipukizi wenye vipaji kutoka ngazi ya klabu.

Kocha huyo aliwataja wachezaji Florent Malouda na Franck Ribery hawatakuwa na muda mrefu kabla ya kustaafu soka na kuongeza kuwa anashangazwa kuona hadi sasa hakuna mrithi wa nyota hao. Malouda ni mshambuliaji tegemeo wa Chelsea na Ribery anacheza klabu ya Bayern Munich.

'Tuna wachezaji wachache wanaocheza klabu kubwa za Ulaya ambao bila shaka wanaweza kuibuka kuwa nyota siku za usoni. Lazima tuwe wakweli kama timu inakuwa na vijana watatu au wanne mahiri ni rahisi kupata mafanikio tofauti na ilivyo sasa, kimsingi tupo mbali sana," alisema Blanc.

Ufaransa iliwahi kutwaa Kombe la Dunia 1998 kabla ya mwaka 2000 kunyakuwa taji la Ulaya. Baadhi ya wachezaji waliounda kikosi hicho ni pamoja na nguli, Didier Deschamps, Zinedine Zidane (Juventus) Marcel Desailly (Chelsea), Patrick Vieira, Emmanuel Petit (Arsenal) na Youri Djorkaeff aliyekuwa Inter Milan.

No comments:

Post a Comment