LONDON, England
MUDA Mfupi baada ya Liverpool kuchapwa mabao 2-0 na Stoke City, kocha Roy Hodgson amesema hatima ya klabu hiyo ipo nje ya uwezo wake kufuatia mashabiki kumzonga kutaka, Kenny Dalglish arudishwe kuinoa timu hiyo yenye makao makuu Anfield.
Mashabiki wa Liverpool, walichukizwa na kipigo hicho na muda mfupi baada ya mpira kumalizika, walitaka kocha wa zamani, Dalglish aliyeipa ubingwa wa England mara ya mwisho mwaka 1990 kuchukuwa mikoba ya Hodgson.
Mabao yaliyofungwa na Ricardo Fuller na Kenwyne Jones yalitosha kumpa homa Hodgson aliyechukuwa nafasi ya Rafael Benitez aliyetua Inter Milan. Kocha huyo wa zamani wa Fulham alisema anahisi kibarua chake kipo shakani baada ya mashabiki hao kumtaka Dalglish.
"Hakuna nililoweza kufanya hapa, nitaendelea kufanya kazi yangu lakini nitakuwa katika mazingira fulani. Kama klabu itakuwa tayari kumleta kocha mwingine nitakuwa tayari kumkabidhi kazi, mashabiki wananipa presha kubwa sijui nini la kufanya" alisema Hodgson.
Awali, beki wa Liverpool, Glen Johnson alitibuana na Hodgson wiki iliyopita baada ya kukosa mbinu za ufundishaji wa kocha huyo mwenye heshima England. Winga wa zamani wa timu hiyo aliyeitumikia Anfield miaka mitatu kabla ya kutua Stoke City, Jermaine Pennant alisema itakuwa ngumu kwa Liverpool kurejea kiwango cha zamani.
"Mashabiki wanataka kuiona Liverpool ya zamani, siyo jambo rahisi. Wachezaji hawana kiwango bora lakini kuna baadhi yao wanapigana kujilinganisha na wale wa zamani itachukuwa muda. Wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kufikia mafanikio kama ya Chelsea au Manchester United," alisema Pennant.
No comments:
Post a Comment