LONDON, England
NAHODHA wa Arsenal Cesc Fabregas hatacheza katika mchezo wa fainali ya Carling Cup Jumapili dhidi ya Birmigham kufuatia kuumia nyuma ya kifundo cha mguu katika mchezo dhidi ya Stoke City Jumatano iliyopita.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alithibitisha kukosekana kwa mchezaji huyo kwenye fainali hiyo katika luninga ya timu hiyo Alhamisi jioni, ingawa alisema hadhani kama maumivu hayo yatakuwa ya muda mrefu.
“Ameumia kidogo lakini atakosa mchezo wa Jumapili,” alisema Mfaransa huyo. “Ni kwa muda gani atapumzika kujiuguza sijui lakini nadhani itakuwa kwa Jumapili tu.
“Amehuzunika. Wote tumesikitika juu ya hilo. Njia pekee ya kumsaidia ni kuhakikisha tunashinda hilo taji kwani ametoa mchango mkubwa katika mashindano hayo.
Pamoja na Fabregas kukosa fainali ya Jumapili, Wenger hawezi kutoa chochote kwa kuheshimu nahodha huyo kuwa fiti kwa ajili ya kupambana na Barcelona Machi 8.
“Ni vigumu kutoa tarehe ya mwisho,” alisema Wenger. “Haiwezekani.”
Theo Walcott pia anatarajiwa kukosa mchezo wa Jumapili baada ya kuumia kifundo cha mguu katika mchezo na Stoke, lakini Kocha huyo anaamini kuwa mchezaji huyo hakuumia sana.
“Nilimuona asubuhi hii,” alisema Wenger. “Alipata maumivu ya kifundo cha mguu yasiyo makubwa sana.
Hatufikiri kama kuna lingine zaidi ya hilo. Naye pia tunamsikitikia. Hatakuwepo katika mchezo wa Jumapili na labda wiki moja au mbili mbele.”
No comments:
Post a Comment