RAIS wa Chama cha Soka nchini Afrika Kusini (SAFA) Kirsten Nematandani amesema hawana budi kuzipokea kwa mikono miwili fainali za Mataifa ya Bara la Afrika zilizohamishiwa nchini humo zikitolewa nchini Libya.
Kirsten Nematandani alisema fainali hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuchangia maendeleo ya soka nchini humo na anaamini mshawasha wa mashabiki wa soka utarejea tena kama ilivyokua kwenye fainali za kombe la dunia pamoja na fainali za wanawake za barani Afrika.
Alisema baada ya kupatiwa nafasi hiyo kinachoendelea kwa sasa ni maandalizi ya viwanja ambavyo vinatakiwa kuwa tayari kabla ya kuanza kwa fainali hizo April 17 na kumalizika May 2.
Hata hivyo amekiri ubora na ubunifu wa hali ya juu ndio vimekua chanzo kwa nchi ya Afrika kusini kushinda nafasi hiyo ambayo pia ilikua ikiwani na nchi nyingine mbili za barani Afrika baada ya kuonekana kwamba fainali hizo za vijana chini ya umri wa miaka 20 haziwezi kufanyika nchini Libya kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo.
Kufuatia hatua ya kuhamishiwa kwa fainali hizo nchini Afrika kusini, timu ya taifa ya nchi hiyo chini ya umri wa miaka 20 imepata nafasi ya kipekee kushiriki baada ya kuenguliwa kwa timu ya taifa ya Libya ambayo haitokua na muda wa kutosha wa kujiandaa.
Fainali hizo zitashuhudia timu nane zilizopangwa kwenye makundi mawili zikiwania nafasi nne za kucheza fainali za kombe la dunia kwa vijana za mwaka huu zitakazofanyika nchini Colombia mwezi June.
Kundi A
Afrika kusini , Mali, Misri pamoja na Lesotho.
Kundi B
Ghana, Nigeria, Cameroon pamoja na Gambia.
No comments:
Post a Comment