KAMATI ya nidhamu ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) inaendelea na shughuli ya kuchunguza kesi ya upangaji wa matokeo katika michezo ya kimataifa ya kirafiki iliyozihusisha nchi kutoka barani Ulaya na kwingineko.
Kamati hiyo inaendelea na shughuli hiyo huku michezo inayochunguzwa ni ile iliyoihusisha timu ya taifa ya Bulgaria dhidi ya Estonia pamoja na Latvia dhidi ya Bolivia iliyochezwa February 9 mwaka huu.
Michezo hiyo ilianza kutiliwa mashaka kutokana na upatikanaji wa matokeo ambapo katika mchezo ulioihusisha timu ya taifa ya Bulgaria dhidi ya Estonia timu hizo zifungana mabao mawili kwa mawili huku Latvia wakiifunga Bolivia mabao mawili kwa moja.
Mabao yote katika michezo hiyo miwili yalipatikana kwa njia ya mikwaju ya penati ambapo upatikanaji wake ulionekana kuwa wa utata hali ambayo ilizua hofu na ndipo uchunguzi wa FIFA ulipochukua mkondo wake.
Michezo hiyo miwili ya kirafiki iliandaliwa na kampuni ya uwakala wa soka ya nchini Urusi ijulikanayo kwa jina la Footy Sport International ambayo pia huenda ikaingia katika sokomoko hilo ambalo linatarajiwa kutolewa maamuzi mazito.
Pamoja na uchunguzi huo kuendelea tayari chama cha soka nchini Hungary kimeshatangza kumfungia muamuzi Kolos Lengyel pamoja na wasaidizi wake wawili kutoka nchini humo kufuatia kuhusishwa na tuhuma hizo za upangaji wa matokeo.
Kamati hiyo ya nidhamu ya FIFA pia itachunguza matokeo ya michezo mingine yanayodaiwa kupangwa ambapo michezo hiyo ni pamoja na ule ulioshirikisha timu ya taifa ya Togo iliyokubali kisago cha mabao matatu kwa sifuri toka kwa Bahrain huku mchezo mwingine ni kati ya timu ya taifa ya Zimbabwe dhidi ya Thailand pamoja na Malaysia iliyochezwa mwaka 2009.
No comments:
Post a Comment