KOCHA wa klabu ya Everton David Moyes ameingiwa hofu kubwa kufuatia kuumia kwa kiungo wa kimataifa toka nchini Hispania Mikel Arteta ambae anadhaniwa huenda ikamchukua muda wa majuma kadhaa kurejea tena uwanjani.
Hofu hiyo kwa meneja huyo wa kimataifa toka nchini Scotland imeibuka usiku wa kuamkia hii leo baada ya mchezaji huo kupata maumivu ya nyama za paja akiwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya soka nchini Uingereza dhidi ya Birmingham City.
Arteta ilimchukua muda wa dakika 8 za mchezo huo uliochezwa huko Goodson Park kabla hajapata maumivu ya nyama za paja ambayo yalipelekea kutolewa nje ya uwanja na nafasi yake kushikwa na Séamus Coleman.
Moyes alisema mchezaji huyo itamchukua muda huo kurejea tena uwanjani kutokana na muonekano wa jeraha lake, lakini hii leo alitarajiwa kufanyiwa vipimio ambavyo vingetoa majibu sahihi ya muda atakaokuwa nje ya uwanja.
Kuumia kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 kunampa mashaka makubwa Moyes kufuatia hali ya kikosi chake hivi sasa kuwa kwenye wakati mgumu kwani tayari ameshawapoteza viungo kama Marouane Fellaini, Tim Cahill pamoja na beki wa pembeni Phil Neville ambao wote ni majeruhi.
Mchezo huo wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza ulimalizika kwa matokeo ya sare ya bao moja kwa moja ambapo kwa upande wa wenyeji Everton bao lao lilipachikwa wavuni na beki John Heitinga katika dakika ya 35 huku bao la Birmingham city likifungwa na Jean Beausejour katika dakika 17.
No comments:
Post a Comment