Thursday, March 10, 2011

PALADINI AITIA MATATANI KUPANDA DARAJA QP RANGERS.

Mwenyekiti wa Queens Park Rangers, Gianni Paladini.

LONDON, England
NDOTO za klabu ya Queens Park Rangers kucheza ligi kuu ya soka nchini Uingereza msimu ujao huenda zikaingia gizani kufuatia uongozi wa klabu hiyo kuvunja sheria za usajili zilizowekwa na FA.

Queens Park Rangers walio kwenye kilele cha msimamo wa ligi daraja la kwanza nchini humo wameingia katika mtiririko huo wa kupoteza malengo yao kufuatia kubainika kwa udanganyifu uliofanywa kwenye usajili wa kiungo wa kimataifa toka nchini Argentina Alejandro Faurlin uliowagharimu kiasi cha paund million 3.4.

Uchunguzi uliofanywa na FA umebaini kwamba kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 alisajiliwa kwa njia ambazo si halali tena kwa kutumika kwa mtu wa pembeni ambae alifanikisha safari yake ya kujiunga na Queens Park Rangers mwaka 2009 akitokea Instituto de Cordoba ya nchini kwao Argentina.

Kufuatia tatizo hilo FA huenda wakaipokonya pointi klabu hiyo hatua ambayo itasababisha kuiengua kileleni na kutoa nafasi kwa klabu nyingine kupanda daraja na kucheza ligi kuu msimu ujao.

Tuhuma kubwa huenda zikamuangukia mwenyekiti wa klabu ya Queens Park Rangers Gianni Paladini anaedaiwa kuwa mstari wa mbele kufoji nyaraka za uhamisho wa mchezaji huyo kwa kushirikiana na wakala wake.

No comments:

Post a Comment