Friday, March 25, 2011

STARS NDANI YA KIBARUA KIZITO NA AFRIKA YA KATI.

Nahodha wa Stars Shadrack Nsajigwa (kushoto), Kocha Mkuu wa Stars Jen Poulsen (katikati) na Kocha wa timu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati Accorsi Jules, wakiongea na waandishi wa habari kuhusu mchezo wao wa kesho. 

DAR ES SALAAM, Tanzania
TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kesho itakuwa na kibarua kizito cha kuivaa timu ya Taifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati katika kutafuta tiketi ya kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hii itakuwa ni nafasi pekee kwa Stars kujaribu nafasi yao haswa ikizingatiwa watakuwa wakicheza mbele ya maelfu ya mashabiki hapa nyumbani ili kujiweka katika nafasi ya kushiriki michuano hiyo.

Timu ya Afrika ya Kati nayo haitakubali kirahisi haswa ikizingatiwa rekodi yao nzuri ya michezo iliyopita ambapo walitoa suluhu na Morocco ugenini kabla ya kuisindilia mabao 2-0 Algeria nyumbani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kocha Mkuu wa Stars Jen Poulsen alisema kikosi chake kimejiandaa vyema na kiko tayari kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa mgumu lakini unaweza kuwa na matokeo mazuri.

Poulsen alisema karibu wiki mbili kikosi chake kimekuwa katika maandalizi kabambe ambapo alisema hakuna tatizo la majeruhi linalomsumbua kwa sasa na wachezaji wamejiandaa vyema kimazoezi na kiakili kwa ajili ya mchezo huo muhimu.

Naye Nahodha wa Stars Shadrack Nsajigwa alisema kwa niaba ya wenzake kwamba wamejiandaa vyema na wako tayari kwa ajili ya mchezo na kuahidi ushindi katika mchezo huo, japo aliwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi ili kuishangilia timu yao.

Mbali na Stars na Afrika ya Kati michezo mingine itakayochezwa kesho ya kutafuta tiketi ya michuano hiyo katika nchi mbalimbali barani Afrika ni kama ifuatavyo:

Chad vs Botswana
Mali vs Zimbabwe
Madagascar vs Guinea
Burkina Faso vs Namibia
Rwanda vs Burundi
Cape Verde vs Liberia
Guinea Bissau vs Uganda
Sudan vs Swaziland
Libya vs Comoros
Niger vs Sierra Leone

No comments:

Post a Comment