KOCHA wa klabu ya Liverpool Kenny Dalglish anaendelea kulifuma zaidi jeshi lake baada ya jana jioni kufanikiwa kumsainisha mkataba mpya kiungo wa kimataifa toka nchini Brazil Lucas Leiva.
Dalglish amefanisha utaratibu huo baada ya kuvutiwa na uchezaji wa kiungo huyo aliejiunga na klabu ya Liverpool mwaka 2007 akitokea nyumbani kwao kwenye klabu ya Gremio kwa uhamisho wa paund million 5.
Kocha huyo wa kimataifa toka nchini Scotland alisema Lucas ni mchezaji mwenye kubadilika kimtazamo chanya tangu alipoanza kukinoa kikosi cha klabu ya Liverpool hivyo anaamini mchezaji huyo ni hazina kubwa kwa hivi sasa pamoja na miaka ijayo.
Kwa upande wake Lucas Leiva alisema hatua ya kusaini mkataba mpya imemuweka katika mazingira mazuri klabuni hapo na kujihisi anathaminiwa kufuatia mchango wake mkubwa anaoutoa akiwa nje na ndani ya uwanja akitetea Liverpool.
Ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa kujituma zaidi tena kwa kushirikiana na wachezaji wengine ili kuweza kutimiza malengo yaliyowekwa na uongozi wa ngazi za juu ya kuhakikisha wanarejea kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao baada ya kukosa nafasi hiyo msimu huu.
Lucas alianza kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Liverpool baada ya kuondoka kwa kiungo wa kimataifa toka nchini Hispania Xabi Alonso pamoja na kiungo wa kimataifa toka nchini Argentina Javier Mascherano.
katika hatua nyingine Dalglish amethibitisha taarifa za kurejea mazoezini kwa kiungo na nahodha wa kikosi chake Steven Garrard ambae alikua nje ya uwanja kwa majuma kadhaa baada ya kufanyiwa upasuaji kufuatia matatizo ya ngiri yaliyokua yakimsumbua.
Alisema kurejea mazoezini kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30 kunatoa nafasi ya asilimia 50 kwa 50 ya kumchezesha katika mchezo wa ligi wa mwishoni mwa juma hili ambapo Liverpool watakua ugenini wakikabiliana na West Bromwich Albion.
Wakati huo huo meneja wa klabu ya West Bromwich Albion ambae alitimuliwa kazi ya kukinoa kikosi cha Liverpool mwishoni mwa mwaka jana Roy Hodgson amesema mchezo huo hatouchukulia kama sehemu ya kulipiza kisasi zaidi ya kuwahimiza wachezaji wake kucheza kwa kujituma kwa minajili ya kuepukana na janga la kurejea kwenye shimo la kushuka daraja msimu huu.
No comments:
Post a Comment