Friday, April 1, 2011

"BADO NIPONIPO SANA HAPA." RAUL

SCHALKE, Ujerumani
MSHAMBULIAJI wa kimataifa toka nchini Hispania Raúl González amesema hana mpango wowote wa kuikacha klabu yake ya sasa ya Schalke 04 ya nchini Ujerumani na badala yake atakuwepo klabuni hapo kama mkataba wake unavyoeleza.

Raúl amelazimika kupasua ukweli huo kufuatia taarifa zinazomuandama kwa sasa ambapo inadaiwa kwamba anajipanga kuondoka huko Veltins-Arena, (Gelsenkirchen) baada ya kukasirishwa na utaratibu uliochukuliwa na viongozi wa ngazi za juu wa kumtimua kazi aliekua meneja Wolfgang-Felix Magath, ambae kwa sasa amerejea kwenye klabu yake ya zamani ya Wolfsburg.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alisema yeye binafsi alisaini mkataba wa kuitumikia klabu ya Shalke 04 hadi mwaka 2012 na hakujiunga na klabu hiyo kwa ajili ya Wolfgang-Felix Magath, ambae amelazimika kuondoka baada ya matokeo mabovu kuendelea kumuandama katika michezo ya ligi ya nchini ujerumani.

Hata hivyo Raúl amedai bado ana nafasi ya kusaidiana na wachezaji wengine klabuni hapo kwa ajili ya kuizawadia Shalke 04 ubingwa wa soka wa kombe la nchini Ujerumani mwishoni mwa msimu huu baada ya kufanikiwa kutinga kwenye hatua ya fainali ya michuano hiyo dhidi ya klabu inayoshiriki ligi daraja la pili nchini humo ya Duisburg.

Mbali na kuwa na ndoto za kuizawadia ubingwa klabu hiyo bado Raúl ana matumaini mengine ya kuhakikisha wanafika mbali katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya baada ya kufanikiwa kutinga kwenye hatua ya robo fainali ambapo watakutana na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Inter Milan.

No comments:

Post a Comment