SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa Kimataifa kati ya timu Taifa ya Tanzania (U23) na timu ya Taifa ya Uganda chini ya miaka 23 (The Kobs) kutafuta tiketi ya kucheza michuano ya Olimpiki 2012, London, Uingereza mchezo utakaocheza katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema maandalizi katika mchezo huo muhimu yako katika hatyua za mwisho.
Alisema viingilio katika mchezo huo vitakuwa kama ifuatavyo; ambapo Jukwaa Kuu (VIP A) kiingilio kitakuwa shs. 10,000, VIP B&C 5,000, Jukwaa la rangi ya kijani, Bluu na viti vya Rangi ya Chungwa vinavyotizamana na VIP na nyuma ya magoli kiingilio kitakuwa shilingi 1,000.
Wambura alisema tiketi zinatarajiwa kuuzwa siku moja kabla ya mchezo katika vituo vya Premier Betting (Kariakoo- Mtaa wa Sukuma, Buguruni Sokoni, Manzese Midizini, JM Mall na Tandale kwa Mtogole), Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Steers (Mtaa wa Ohio na Samora), Big Bon Msimbazi (Kariakoo) na Uwanja wa Uhuru.
The Kobs inatarajia kuwasili nchini Alhamisi Aprili 28 mwaka huu saa 10.30 jioni kwa ndege ya Uganda Air na kurejea nyumbani Jumapili Mei 1 saa 11.50 kwa ndege hiyo hiyo.
Msafara wa timu hiyo utaongozwa na Ofisa wa Shirikisho la Soka nchini Uganda (FUFA) Sam Lwere na utafikia hoteli ya Durban iliyoko Barabara ya Uhuru, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment