UONGOZI wa mabingwa wa soka nchini Ureno FC Porto umesema hautokuwa na kinyongo endapo kocha wa timu hiyo Andre Villas-Boas ataondoka kufuatia kuhusishwa na taarifa za kuwa mbioni kuajiriwa na klabu ya Chelsea ya Uingereza.
Porto walisema taratibu za kuondoka kwa kocha huyo zinajulikana na kikubwa ni kulipwa fedha ambazo zinatokana na hatua ya kuvunjwa kwa mkataba wake klabuni hapo.
Mwishoni mwa juma lililopita, Porto waliutaka uongozi wa klabu ya Inter Milan kulipa paund million 13 endapo wangehitaji kumchukua Villas-Boas ambae ameweka rikodi ya kutwaa ubingwa wa ligi ya barani Ulaya akiwa kocha mwenye umri mdogo.
Hata hivyo Chelsea endapo wanahitaji kumuajiri meneja huyo mwenye umri wa miaka 33 kwa ajili ya kuziba nafasi ya Carlo Ancelotti watatakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha.
Chelsea wanahusishwa na taarifa za kutaka kumchukuwa Villas-Boas baada ya majuma kadhaa kupita ambayo yalishuhudia klabu hiyo ya London ikihusishwa na taarifa za kutaka kumrejesha Stamford Bridge Guus Hiddink ambae kwa sasa ana mkataba wa kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Uturuki ambacho kinawania nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya barani Ulaya.
Endapo itakua hivyo, Chelsea wataweka historia ya kumuajiri kwa mara nyingine meneja wa klabu ya Porto aliepata mafanikio katika ligi ya nyumbani pamoja na ligi ya barani Ulaya, ambapo kwa mara ya kwanza walifanikiwa kumchukua Jose Mourinho ambae aliiwezesha klabu hiyo ya Estádio do Dragão kutwaa ubingwa wa ligi ya nyumbani pamoja na ligi ya mabingwa barani Ulaya na hiyo ilikua mwaka 2004 .
No comments:
Post a Comment