Sunday, August 29, 2010

AC MILAN YAMNYAKUA IBRAHIMOVIC

Klabu ya AC Milan ya Italia imefanikiwa kumnyakuwa mshambuliaji wa kimataifa Msweden Zlatan Ibrahimovic kutoka klabu ya Barcelona.


Juhudi za Makamu wa Rais wa Milan Adriano Galliani kubakia mjini Barcelona kuendeleza mazungumzo ya kumyakua mchezaji huyo wa zamani wa mahasimu wao Inter Milan hatimaye zilizaa matunda jana.

Kazi kubwa imeshakamilika kwa Rais wa Milan Silvio Berluscon ambaye mwezi uliopita alisema kama kuna umuhimu wowote wa kusajili mchezaji nyota katika kikosi chake angefanya hivyo.

"AC Milan wanatangaza kuwa tayari wameshamnyakua Ibrahimovic kutoka Barcelona kwa mkopo lakini wakiwa wana uwezo wa kumnunua baadaye katika msimu wa 2010/2011 kwa ada ya euro milioni 24" ilisema taarifa kutoka tovuti ya klabu.

Taarifa hiyo pia iliendelea kusema kuwa mchezaji atafanyiwa vipimo vya afya Jumatatu na baadae atasaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo.

"Ndio tayari tumeshamchukua kwa mkopo lakini tukiwa na uwezo wa kumnunua kwa kiwangi hicho cha pesa na Jumatatu atasaini mkataba. Kiwango hicho cha pesa kitalipwa kwa kipindi cha miaka mitatu kila mwaka euro milioni 8. naishukuru Milan pamoja na Rais Berluscon kwa ushirikiano walionyesha katika hilo" Galliani aliwaambia waandishi wa habari Barcelona.

Naye Ibrahimovic alisema kuwa klabu yake hiyo mpya ni klabu bora duniani, na huwa inafanya mashambulizi ya kuvutia.

"Mimi ni mchezaji wa Milan sasa. Nina furaha kwamba kila kitu kimekwenda vizuri. Walikuwa na msimu wa kuvutia msimu uliopita, na sina la kusema kuhusu mashabiki wa Inter" alisema Ibrahimovic.

"Uhamisho huu umeniongezea morali. Nimekuja hapa kushinda michuano ya klabu bingwa ya Ulaya (Champions League), nahitaji kushinda mara mbili" alimalizia Ibrahimovic.

Kwa bei waliomyakuwa mchezaji huyo Milan watakuwa wamepiga bao kwa kumchukua mchezaji huyo kwa bei ya chee baada ya Barcelona kumnunua kutoka Inter kwa euro milioni 66 msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment