ROME, Italia
AC Milan imeanza msimu mpya kwa kishindo kwa kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Lecce ambapo mshambuliaji mpya Zlatan Ibrahimovic alishuhudia mchezo huo Uwanja wa San Siro.
Ibrahimovic ametua AC Milan akitokea Barcelona na juzi alitambulishwa kwa heshima mbele ya mashabiki wa klabu hiyo. Nyota huyo wa zamani wa Inter Milan.
Nahodha huyo wa Sweden alipita mbele ya zulia jekundu kabla ya kutambulishwa. "Nimekuja hapa kushinda, mwaka huu utakuwa wa ushindi kwa kila jambo," alisema Ibrahimovic aliyekuwa amekaa jirani na mmiliki wa AC Milan, Silvio Berlusconi.
Alexandre Pato alikuwa wa kwanza kumpa raha Ibrahimovic kwa kufunga mabao mawili, Thiago Silva na nguli wa Italia, Filippo Inzaghi walichangia ushindi huo kwa kufunga bao moja kila mmoja. Inzaghi, alifunga bao lake la 154.
Kocha mpya wa AC Milan, Massimiliano Allegri alisema amefurahi timu hiyo imeanza ligi kwa ushindi na alidokeza Ibrahimovic ataanza kuitumikia klabu hiyo katika mchezo dhidi ya Cesena baada ya kufanya mazoezi siku 14.
Allegri anatarajiwa kupata mtihani mgumu kupanga safu ya ushambuliaji baada ya kumsajili Ibrahimovic atakayechuana na Pato, Ronaldinho, Marco Borriello na Inzaghi kuwania namba. Katika mechi zingine za Italia, Juventus ilishinda bao 1-0 dhidi ya Bari.
Napoli ilitoka sare bao 1-1 na Fiorentina, Sampdoria iliichapa Lazio 2-0, Chievo Verona ilipata ushindi wa mabao 2-1 ilipovaana na Catania. Palermo ilitoka suluhu na Cagliari 0 wakati Parma iliinyuka Brescia mabao 2-0 na AS Roma ililazimishwa suluhu na Cesena.
No comments:
Post a Comment