MABONDIA wa timu ya Taifa ya Ngumi za Ridhaa wataendelea na mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Jumuiya ya Madola inayotarajiwa kufanyika baadaye Octoba mwaka huu, Delhi, India.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa nchini (BFT), Makore Mashaga alisema wamefikia hatua hiyo ili kutoingilia mipango ya kocha ambayo alikwishaiandaa.
Alisema wakati mabondia hao wakiendelea na mazoezi Kamati Maalumu iliyoundwa na BFT kuchunguza tukio la mgomo wa mabondia hao katika mashindano ya East Afrika Mabingwa wa Mabingwa nayo itaendelea na kazi yake kama kawaida.
Alisema mara baada ya kamati hiyo kumaliza uchunguzi wake itawafikishia taarifa pamoja na kuwashauri hatua za kuchukua halafu ndipo kamati ya utendaji na yenyewe itakaa na kuamua la kufanya.
"Unajua mashindano ya jumuiya ya madola yapo karibu sana ndio maana tunakuwa makini katika suala hili ili tusije kuvuruga mipango ya mwalimu aliyoipanga kwa ajili ya timu hiyo" aliongeza Mashaga.
Mabondia hao waligomea mashindano hayo kutokana na kile walichodai kuwa uongozi wa BFT ulikuwa hauwajali kwa kuwanyima baadhi ya mahitaji muhimu.
Moja ya mahitaji ambayo walikuwa wakidai ni kwa wageni kuwekwa kambini ili wao wakiambia waende kula majumbani kwao na kurudi ulingoni kuendelea na mashindano.
No comments:
Post a Comment