KOCHA wa timu ya soka ya Temeke United (TMK United), itakayoshiriki michuano ijayo ya Ligi ya soka Daraja la Kwanza, Keneth Mwaisabula ana hofu kuwa klabu yake imepangwa kwenye kundi gumu.
Kocha huyo mkongwe nchini ambaye amejiunga na kikosi hicho msimu huu kuchukua nafasi ya Fred Felix 'Minziro', aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam alipokua akizungumzia ushiriki wa timu hiyo kwenye ligi.
Mwaisabaula alisema TMK united ambayo ilikua miongoni mwa klabu tisa, ambazo zilicheza fainali za ligi hiyo msimu uluiopita kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na kushindwa kupanda daraja msimu huu imepangwa kundi A.
Kundi hilo pia lina timu zingine za Manyema Rangers, Villa Squad (Dar es Salaam), Burkinafaso (Morogoro) na Polisi (Iringa).
"Ugumu wa kundi langu nikilinganisha na makundi mengine unatokana na kuwa kuna klabu mbili, ambazo tayari zilishawahi kucheza Ligi Kuu. Hivyo nadhani zenyewe zitakua na uzoefu mkubwa na bila shaka zitatupa ushidani mkubwa," alisema.
Alisema lakini pamoja na kuweko kwa hali hiyo amewaandaa vizuri wachezaji wake, kwani alisema atahakisha vijana wake wanacheza kwa ushindani ili hatimaye wazishinde timu hizo na kupanda na kucheza ligi kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Kulingana na ratiba ambayo imetolewa mwishoni mwa wiki ligi hiyo ambayo itapandisha timu nne, imepangwa kuanza Setemba 4, mwaka huu kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Makundi mengine na klabu shiriki katika mabano ni Coastal Union ya Tanga, Nyerere FC ya Kilimanjaro, Morani FC ya Manyara, Bishop FC ya Arusha, Tanzania Prisons ya Mbeya na Transit Camp ya Dar es Salaam (B).
Zingine ni Oljoro JKT ya Arusha, Mwanza United ya Mwanza, Rhino FC ya Tabora, Polisi ya Morogoro, Polisi ya Tabora na 94KJ ya Dar es Salaam (C).
Ligi hiyo imepangwa kuchezwa kwenye viwanja vya Uhuru (Dar es Salaam), Sheikh Amri Abeid (Arusha),Jamhuri (Morogoro), Ushirika (Moshi), Samora (Iringa), Mkwakwani (Tanga), CCM Kirumba (Mwanza), Ally Hassan Mwinyi (Tabora) na Jamhuri (Dodoma).
No comments:
Post a Comment