Tuesday, August 31, 2010

RAGE ALIDAI GAZETI FIDIA YA BILIONI MOJA.


UONGOZI wa Klabu ya Simba umelipeleka mahakamani gazeti moja binafsi na kulidai shs. bilioni moja kwa kuchapisha habari za uzushi na uchonganishi kuhusu klabu hiyo.

Kauli hiyo imekuja kufuatiwa gazeti la Mwanaspoti ambalo hutoka kila wiki kuchapisha habari katika toleo namba 1070 la Agosti 28-30 lililokuwa na kichwa cha habari kinachosema "Siku 110 za Rage na porojo zake Simba", "Rage ni yule yule hajabadilika".

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage alisema uongozi umesikitishwa na taarifa hizo zilizotolewa na gazeti hilo kwani ni za uzushi na za kupotosha.

Alisema habari hiyo ambayo ilisomeka katika kurasa za 6 na 8 ilikuwa kuaibisha taaluma ya uandishi wa habari za michezo na uvunjwaji wa sheria za nchi kwa kuandika matusi ambayo yaliyoelekezwa kwa uongozi wa Simba na Mwenyekiti wake.

"Toka tuingie uongozi mpya uingie madarakani tumekuwa tukijitahidi kuwa na mahusiano mazuri na vyombo vya habari isipokuwa vyombo vichache vyenye tabia ya kuandika habari zisizo na ukweli zenye lengo lakuturudisha nyuma" alisema Rage.

Alisema kutokana na hilo Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ilikutana hivi karibuni na kuona kwamba kuna umuhimu wa kuchukua hatua za kisheria kwa kudai kuombwa msamaha kwa kudhalilishwa huko na fidia ya shs. bilioni moja.

"Kamati ya utendaji ambayo ilikutana chini ya Makamu Mwenyekiti Godfrey Nyange ililipa suala hili umuhimu kwa kuwa waliona ni habari za udhalilishaji zina lengo la kubomoa uongozi wa klabu, wanachama pamoja na mashabiki wa klabu ndio maana wakaamua kuchukua hatua za kisheria" aliongeza Rage.

Alisema suala hilo litakuwa ni mara ya mwisho kuongelewa na uongozi wa klabu hiyo kwenye vyombo vya habari kwa sababu sheria imeshaanza kuchukua mkondo wake.

No comments:

Post a Comment