Tuesday, August 31, 2010

VENUS AANZA VYEMA US OPEN.

Akicheza mechi ya kwanza baada ya miezi miwili, mchezaji tenisi nyota wa Marekani, Venus Williams alimshinda mpinzani wake, Roberta Vinci kutoka Italia kupata ushindi wa seti 6-4, 6-1 katika michuano ya U.S. Open raundi ya pili.


Venus alitakiwa kupumzika baada ya kuumia goti la kushoto baada ya kupata maumivu Juni 29 katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Wimbledon. Katika mchezo huo, nyota huyo nambari tatu kwa ubora duniani, alionyesha kiwango bora kabla ya kupata ushindi huo.

Katika mchezo mwingine, mchezaji wa zamani nambari moja kwa ubora duniani, Ana Ivanovic alipenya raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kushinda seti 6-3, 6-2 dhidi ya Ekaterina Makarova anayeshikilia nafasi ya 52 kwa viwango. Ana alishika nafasi hiyo baada ya kung'ara mwaka 2008.

Mserbia huyo aliyeporomoka kwa viwango vya ubora hadi kufikia nafasi ya 40, alifanya kazi ya ziada kupata ushindi huo baada ya mpinzani wake kutoa upinzani. Mwaka 2008, aliishia raundi ya pili. Tangu michuano ya U.S Open ianzishwe mwaka 1968, hakuna mwanamke aliyekuwa akishikilia nafasi ya kwanza kutupwa nje hatua ya awali.

"Jambo la msingi kwangu nimefurahi nimerejea katika kiwango, ni mwanzo mzuri wa michuano. Nimejitahidi kudhibiti baadhi ya presha na haya ni matokeo mazuri kwangu," alisema mchezaji huyo.

No comments:

Post a Comment