Tuesday, August 31, 2010

YOBO ATIMKIA WEST HAM.

LONDON, England

BEKI wa Everton Joseph Yobo amemfuata mshambuliaji nyota wa Nigeria, Obinna Nsofor baada ya kuihama Everto na kutua klabu ya West Ham United muda mfupi kabla ya msimu wa usajili wa majira ya kiangazi kufikia ukingoni.

Nahodha huyo wa zamani wa Nigeria, amejiunga West Ham kwa mkopo wa miezi sita. Wiki iliyopita Nsofor alikamilisha usajili wa kutua London baada ya kutia saini mkataba wa muda mrefu akitokea kwa mabingwa wa Ulaya Inter Milan.

Mchezaji huyo alijiunga Everton kwa mkopo mwaka 2002 kutoka klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa. Yobo ametimia West Ham baada ya kukosa namba kikosi cha kwanza na huenda beki huyo wa kati akaongeza mkataba wa muda mrefu ili apate nafasi ya kulinda kiwango chake.

Yobo (29) tayari amejiunga na kambi ya timu ya taifa Nigeria 'Super Eagles' inayojiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ambapo kikosi hicho kitashuka uwanjani mwishoni mwa wiki kuvaana na Madagascar mjini Abuja.

Kabla ya kupata mtihani wa namba kikosi cha kwanza, mchezaji huyo alikuwa beki tegemeo wa Everton tangu alipotua Goodson Park. Yobo alikwenda Afrika Kusini na Nigeria kushiriki fainali za Kombe la Dunia ambapo timu hiyo iliboronga. Katika michuano hiyo Hispania ilitwaa kombe baada ya kuifunga Uholanzi bao 1-0.

No comments:

Post a Comment