ROME, Italia
MABINGWA wa Italia, Inter Milan jana walitoka uwanjani vichwa chini baada ya kulazimishwa suluhu na Bologna katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi Kuu (Serie A) nchini humo.
Matokeo hayo yalionekana kumkasirisha kocha mpya wa mabingwa hao wa Ulaya, Rafael Benitez aliyewashukia wachezaji wake akidai walicheza kizembe na kuchangia kupata matokeo hayo ya kushangaza. Mahasimu wao wakubwa AC Milan, walianza vyema baada ya kuikandamiza Lecce mabao 4-0.
Bologna ilicheza mchezo huo bila kocha Franco Colomba aliyetimuliwa na rais wa klabu hiyo Sergio Porcedda. Kocha msaidizi wa kikosi hicho Paolo Magnani, alikuwa kwenye benchi na kushuhudia vijana wake wakitoa upinzani kwa mabingwa hao licha ya Rafael Benitez kucheza wachezaji nyota.
Nahodha wa Cameroon, Samuel Eto'o alifanya kazi kubwa kuipenya ngome ya Bologna kutafuta mabao lakini mashuti yake makali hayakuzaa matunda. Kipa wa timu hiyo, Emiliano Viviano alikuwa nyota wa mchezo baada ya kuokosa kwa ustadi mabao ya Inter Milan.
Benitez aliyechukuwa nafasi ya Jose Mourinho aliyetua Real Madrid, alitumia mfumo wa 4-4-3, lakini Inter Milan ilishindwa kufua dafu mbele ya wenyeji wao ambao walicheza mchezo wa nguvu muda wote. Kocha huyo wa zamani wa Liverpool alimsifu Viviano akidai aliwanyima ushindi kwa kuokoa mabao mengi.
Mkenya, McDonald Mariga alifumua shuti lililogonga mwamba baada ya kupata pasi ya Esteban Cambiasso. Kipa, Viviano alifanya kazi ya ziada kwa kuokoa mpira uliopigwa na kiungo Wesley Sneijde dakika 73 kuokoa kwa kichwa. Eto'o, alipiga shuti umbali wa yadi mbili lakini Viviano aliokoa.
No comments:
Post a Comment