WINGA machachari wa klabu ya Arsenal Theo Walcott ameendelea kuonyesha kiwango cha juu kwa kuzifumania baada ya kufunga bao dhidi ya Blackburn Rovers na kufanya kuwa na mabao manne katika mechi mbili za ligi alizocheza.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 21 aliipatia Gunners goli la kuongoza wakati timu hiyo iliposhinda jumla ya mabao 2-1 na kuvunja mwiko uliodumu takribani miaka nane kutokuifunga timu yoyote iliyo chini ya Sam Alladyce ambaye ndio kocha wa Rovers hivi sasa.
"Msimu uliopita tulipata matokeo ya kukatisha tamaa. Rovers walicheza mchezo mzuri na walikuwa wagumu kufungika haswa ikizingatiwa kuwa walikuwa nyumbani" alisema Walcott baada ya mchezo wao huo.
Walcott alifunga mabao matatu (hat-trick) mwisho wa wiki iliyopita dhidi ya Blackpool na anashukuru kurudi katika kiwango chake baada ya kuachwa katika kikosi cha England kilichoshiriki Kombe la Dunia Juni mwaka huu.
"Sikumlaumu yoyote, kwani nilifikiri vizuri, nilipata muda mzuri wa kupumzika na sasa nataka kuonyesha kitu gani naweza kufanya" aliongeza Walcott.
"Majeruhi yalinisumbua sehemu kubwa ya msimu uliopita. Msimu huu nataka kucheza kwa nguvu zangu zote na kujaribu kufunga magoli kila mara"
Naye mlinda mlango wa Gunners Manuel Almunia amefurahishwa na matokeo hayo dhidi ya Rovers na anaamini kwamba timu yake imeonyesha kiwango kizuri haswa sehemu ya ukabaji baada ya kushindwa kumudu mashambulizi ya Blackburn msimu uliopita.
"Baada ya kushinda unaweza kusema kwamba tulionyesha kiwango kizuri upande wa ukabaji. Timu yao ilikuwa nzuri lakini vijana wetu walifanya vizuri leo" Alisema Almunia.
No comments:
Post a Comment