Wednesday, September 29, 2010

AFRIKA KUSINI YAJITOSA KINYANG'ANYIRO CHA KUANDAA AFCON 2015.

JOHANNESBURG, Afrika Kusini
KWA mujibu wa gazeti la Sowetan la Afrika Kusini , Shirikisho la Soka la nchi (SAFA) hiyo tayari limeshatuma barua Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuhusu nia yao ya kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika 2015.

Mara ya mwisho nchi kuandaa michuano hiyo ilikuwa ni mwaka 1996, ambapo Bafana Bafana walichukua ubingwa wa michuano hiyo baada ya kuifunga Tunisia katika mchezo wa fainali.

Taarifa hiyo ilisema Rais wa SAFA Kirsten Nematandani alituma maombi hayo CAF Jumanne baada ya kuamuliwa katika kikao cha menejimenti kilichokaa Johannesburg kitu ambacho kilichangiwa kwa kiasi kikubwa na mafanikio waliyopata katika Kombe la Dunia.

"Bado tunafurahia mafanikio tuliyopata katika Kombe la Dunia na tunategemea itatusaidia katika kushinda mchakato wa kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika. Kutakuwa hakuna maswali kuhusu miundo mbunu kwa kuwa tayari ipo hapa, malazi yapo. Kutakuwa hakuna maswali kuhusu usafiri kwa sababu upo, viwanja bora pia vipo hapa. Tuna kila kitu. Tutaongea na serikali kuhusu wazo letu hili," alikaririwa akisema Nematandani.

Michuano inayofuata itaandaliwa kwa pamoja na Gabon pamoja na Equatorial Guinea 2012 na mwaka utakaofuatia wakati mashindano hayo yatakapobalidilishwa na kuwekwa katika miaka isiyogawanyika itafanyika Libya.

No comments:

Post a Comment