Monday, September 27, 2010

ALMUNIA KUKOSA MECHI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA.

KOCHA wa Arsenal Arsene Wenger amesema kuwa mlinda mlango wake namba moja katika kikosi hicho Manuel Almunia ni majeruhi na hatakuwemo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya huko FK Partizan wiki hii.

Mlinda mlango huyo kutoka Hispania aliumia kisukusuku au kipepsi Jumamosi wakati timu hiyo ilipokubali kichapo dhidi ya timu ya West Bromwich Albion, na nafasi yake inaweza kuzibwa na Lukasz Fabianski.

"Tutamkosa Almunia. Ana matatizo ya kisukusuku. Aliyapata wakati akidaka penati Jumamosi," alisema Wenger. "Pia Kieran Gibbs atafanyiwa majaribio katika mazoezi leo."

Almunia amekuwa akilaumiwa kutokana na mchezo wa Jumamosi ambapo anatuhumiwa kufanya makosa mawili ambayo yaliigharimu timu katika kipindi cha pili lakini Wenger amekanusha uvumi huo akisema angemchagua katika kikosi chake kama asingekuwa ameumia.

"Hapana," alijibu Wenger alipoulizwa kama alimuacha Almunia kutokana na makosa aliyofanya.

"Siku zote wakati timu inaposhindwa wa kwanza kulaumiwa anakuwa golikipa. Lakini huwa tunashinda pamoja na kushindwa pamoja hata kama watu wanakiri alifanya makosa tulipofungwa bao la pili." alimalizia Wenger.

No comments:

Post a Comment