Wednesday, September 29, 2010

ARSENAL, CHELSEA ZAENDELEZA UBABE LIGI YA MABINGWA.

ARSENAL jana imelinda rekodi yake ya ushindi wa asilimia mia moja katika kundi H baada kushinda mabao 3-1 dhidi ya timu ngumu ya Partizan Belgrade ya Serbia, huku golikipa Lukasz Fabianski akiokoa mkwaju wa penati dakika za mwisho.

Arsenal walianza kupata bao ushindi kupitia kwa mchezaji Andrei Arshavin ambaye baadae alikosa penati, mabao mengine ya Arsenal yalifungwa na Marouane Chamakh na Sebastian Squillaci huku bao la kufutia machozi la Belgrade likifungwa na Cleo.

Kabla ya mchezo kuanza, kulitokea matatizo ya kiufundi katika baadhi ya taa za pembeni kushindwa kuwaka kitu ambacho kilitishia mchezo huo kuahirishwa, lakini mwishoni mwamuzi alipokea iliyomruhusu kuendelea na mchezo huo mkwa wakati.

wakati huohuo Chelsea jana walishika usukani wa kundi F baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika Uwanja wa Stamford Bridge. Pamoja na kumkosa mshambuliaji wake tegemeo Didier Drogba na Frank Lampard, vijana wa Carlo Ancelotti waliweza kuwashinda mabingwa hao wa Ufaransa kwa mabao yaliyofungwa na John Terry na Nicolas Anelka.

Katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya mchezo huo, Ancelotti aliwasihi wachezaji wake kusahau mchezo wa ligi walioupoteza dhidi ya Manchester City mwishoni mwa wiki. Ambapo Terry alimjibu kocha wake huyo kwa kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Florent Malouda dakika saba toka mchezo huo uanze, kabla ya Anelka kuongeza la pili kwa mkwaju wa penati baada ya Stephane M'Bia kuunawa mpira uliopigwa na Michael Essien katika eneo la hatari.

Angel Di Maria aliipatia timu yake ya Real Madrid ushindi katika dakika za mwisho dhidi ya Auxerre na kufanya timu kuongoza kundi G.

Mara ya mwisho Madrid kushinda kombe la Klabu Bingwa ilikuwa ni mwaka 2002 wakati Zinedine Zidane alifunga bao kwa staili ya kipekee dhidi ya Bayer Leverkusen katika Uwanja wa Hampden Park, Glasgow. Wamewekeza kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri katika ligi hiyo pamoja na Ligi Kuu ya nyumbani, na mchezaji ambaye walimsajili kutoka Benfica msimu huu ndiye aliyewaokoa huko Ufaransa, kwa kuukwamisha mpira wavuni kwa ufundi mkubwa baada ya mchezaji mwenzake ambaye naye amesajiliwa msimu huu Mesut Ozil kumpatia pasi safi kwenye dakika ya 81 na kuibuka kwa ushindi huo mwembamba wa bao 1-0.

AC Milan ambao walifunga Auxerre katika mchezo wa kwanza, walijikuta wakivutwa shati na Ajax ya Uholanzi kwa kutoka nao sare ya bao 1-1. Mounir El Hamdaoui ndiye aliyefunga bao la kuongoza Ajax dakika ya 23 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Luis Suarez, lakini shujaa wa zamani wa Ajax Zlatan Ibrahimovic alisawazisha bao hilo dakika 15 baadae kwa kusaidiana vyema na aliyekuwa kipenzi cha mashabiki wa Uholanzi Clarence Seedorf.

AS Roma walituliza maumivu ya kufungwa na Bayern Munich katika mchezo wa kwanza wa kundi E kwa kuwafunga CFR Cluj mabao 2-1. Mabao hayakupatikana mpaka katikati ya kipindi cha pili, ambapo beki Philipe Mexes aliipatia timu yake bao la kuongoza kwa shuti kali dakika ya 69 na Marco Borriello aliongeza la pili dakika mbili baadae. Cluj walijibu mapigo dakika saba baadae wakati Ionut Rada alipotumbukiza nyavuni mpira wa kichwa na kupata bao lakufutia machozi.

Bayern walilikuja kutoka nyuma na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Basel, ambao walianza kuongoza katika dakika ya 17 kwa bao lilifungwa na alexander Frei. Bayern walirudisha bao hilo kwa njia ya penati iliyofungwa na Bastian Schweinsteiger katika dakika ya 56, baada ya Thomas Muller kufanyiwa madhambi na Benjamin Huggel, na dakika moja kabla ya mpira kumalizika Schweinsteiger aliipatia timu yake bao la kuongoza.

Katika michezo mingine iliyochezwa jana Shakhtar Donetsk waliifunga Braga mabao 3-0 huku Spartak Moscow nao wakishinda mabao 3-0 dhidi ya Zilina.

No comments:

Post a Comment