Wednesday, September 22, 2010

BENTO AMRITHI QUEIROZ URENO.

LISBON, Ureno
PAULO Bento ametangazwa kocha mpya wa Ureno kuchukuwa nafasi ya Carlos Queiroz aliyefungiwa miezi sita baada ya kupatikana na hatia ya kuwatolea lugha isiyofaa madaktari waliotaka kuwapima wachezaji wa timu hiyo dawa za kuongeza nguvu muda mfupi kabla ya kwenda Afrika Kusini kushiriki Kombe la Dunia 2010. 

Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Ureno mwenye miaka 41, ametia saini mkataba wa miaka miwili hadi Julai 2012. Kabla ya kustaafu soka, Bento alicheza mechi 35 akiwa na timu ya taifa. Bento jana alitambulishwa rasmi mbele ya waandishi wa habari makao makuu ya Shirikisho la Soka Ureno (PFF).

Bento atasaidiwa na Leonel Pontes, Joao Aroso atakuwa kocha wa viungo wakati Ricardo Peres ameteuliwa kufundisha makipa. Kabla ya kutwaa mikoba, benchi hilo la ufundi liliwahi kufanya kazi chini ya Bento kuinoa klabu ya Sporting Lisbon kati ya mwaka 2005 na 2009.

Kabla ya kutundika daluga, Bento alianza kung'ara katika mchezo wa soka akiwa na miaka 17 alipokuwa mchezaji tegemeo wa klabu za Sporting Lisbon na baadaye Benfica. Alikuwa miongoni mwa wachezaji waliocheza fainali za Kombe la Ulaya 2000 na Kombe la Dunia 2002.

"Paulo Bento na benchi la ufundi wametia saini mkataba wa hadi Julai 2012," ilisema sehemu ya mtandao wa Shirikisho hilo. Kocha huyo ataiongoza Ureno katika mechi za kufuzu fainali za Kombe la Ulaya 2012.

Queiroz alifukuzwa siku mbili baada ya kufungiwa miezi sita baada ya Ureno kuchapwa bao 1-0 na Norway katika mechi za kufuzu Kombe la Ulaya 2012.

Ureno ilianza kwa sare ya mabao 4-4 na Cyprus katika mechi za kufuzu fainali hizo. Ureno inashika mkia katika msimamo wa kundi H ikiwa tayari imezidiwa pointi tano na vinara Norway. Mtihani wa kwanza kwa Bento utakuwa Oktoba 8, Ureno itakapokuwa nyumbani kuvaana na Denmark kabla ya kuivaa Reykjavik siku nne baadaye.

No comments:

Post a Comment