MWAMUZI wa zamani anayechukiwa nchini Italia toka fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Japan na Korea Kusini 2002 amekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa JF Kennedy kwa kukutwa na madawa ya kulevya aina ya heroin akiwa amejifunga mwilini mwake.
Maofisa wa Uhamiaji wa nchi hiyo pamoja na maofisa wa forodha walimkamata Byron Moreno Jumatatu baada ya kuwasili New York kwa ndege ya abiria akitokea Ecuador.
Wakati akikaguliwa, Moreno alionekana akitetemeka kwa mujibu wa maelezo ya mahakama ya Brooklyn.
Ofisa wa Forodha alihisi "kitu kigumu katika tumbo la Moreno, kwa nyuma na katika miguu yote miwili," alisema mwendesha mashitaka. Baada ya kumvua nguo na kumkagua walimkuta na mifuko kumi ya plastiki ambayo ilikuwa na madawa ya kulevya yanayokadiriwa kuwa kama kilo 10 hivi, alisema.
Jaji alimpeleka rumande Moreno bila ya dhamana kwa kosa la kukutwa na madawa hayo.
"Naangalia tukio lenyewe ilivyo ili nione ni jinsi gani naweza kumsaidia" alisema mwanasheria Michael Padden anayemwakilisha Moreno Jumanne.
Moreno aliwachanganya mashabiki wa Italia 2002 baada ya kumtoa Francesco Totti, kwa kumpa kadi ya pili ya njano kwa kujirusha katika eneo la hatari dakika 13 kabla ya mpira kumalizika ambapo Italia ilifungwa mabao 2-1 na South Korea katika raundi ya pili ya Kombe la Dunia.
Bao la dakika ya 111 lililofungwa na Damiano Tommasi ambalo lingeweza kuivusha Italia lilikataliwa kwa madai mchezaji huyo alikuwa ameotea, na South Korea walizawadiwa penati ambayo iliokolewa na golikipa Gianluigi Buffon kwa faulo ambayo ilichezwa na Christian Panucci dhidi ya Seol Ki-Hyeon.
"Nafikiri Moreno tayari alikuwa alikuwa na madawa ya kulevya 2002, lakini sio kwenye nguo yake ya ndani bali ndani ya mwili," alikaririwa Buffon akisema kwa utani, "watu wa kichezo wanapojiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya wanapoteza maana ya michezo, ambayo pia inamaana ya kuokoa watoto wa mitaani kwenye hatari kama ya kujihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya.
No comments:
Post a Comment