BERLIN, Ujerumani
NAHODHA wa zamani wa Ujerumani, Lothar Matthaus (49) ametangazwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Bulgaria baada ya kukubali kutia saini mkataba wa mwaka mmoja kuchukuwa nafasi ya Stanimir Stoilov.
Rais wa Shirikisho la Soka Bulgaria (BFU), Borislav Mihaylov alithibitisha kuwa nguli huyo wa zamani aliyecheza kwa mafanikio makubwa Ujerumani na klabu za Ulaya na walitaka kumpa mkataba wa muda mrefu kabla ya Matthaus kukubali kuinoa Bulgaria miezi 12.
Matthaus aliinoa Hungary mwaka 2004-2005, amewahi kuzifundisha klabu mbalimbali za Ulaya ikiwemo Rapid Vienna ya Austria. Mtihani wake wa kwanza utakuwa Oktoba 8, Bulgaria itakapovaana na Wales katika mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Ulaya 2012 ambapo imepangwa kundi G.
Bulgaria ilianza vibaya kampeni yake baada ya kukubali kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya England Septemba 3 kabla ya kuchapwa bao 1-0 ikiwa nyumbani ilipovaana na Montenegro siku nne baadaye. Matokeo hayo yalimfanya Stoilov kutangaza kujiuzulu.
Rekodi ya mkongwe huyo inaonyesha alicheza mechi 150 za kimataifa na aliing'arisha Ujerumani katika fainali za Kombe la Dunia 1990, alikuwa mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia 1991.
Matthaus alistaafu soka akiwa na klabu ya Borussia Monchengladbach, lakini muda mrefu amekuwa mwakilishi wa Bayern Munich. Nguli huyo amewahi kuzinoa klabu za (Rapid Vienna, Austria), (Partizan Belgrade, Serbia), (Atletico Paranaense, Brazil), (Red Bull Salzburg, Austria) na Maccabi Netanya ya Israel.
No comments:
Post a Comment