LISBON, URENO.
KOCHA wa timu ya taifa ya Ureno, Carlos Queiroz amefungiwa miezi sita baada ya kupatikana na hatia ya kutoa lugha isiyofaa kwa madaktari waliotaka kuwapima wachezaji dawa za kuongeza nguvu michezoni kabla ya kwenda Afrika Kusini kushiriki Kombe la Dunia 2010.
Taasisi ya michezo ya Ureno, tayari ilimfungia Queiroz (57) mwezi mmoja lakini ilidai itachukuwa hatua zaidi endapo kutapatikana ushahidi wa kutosha kwamba kocha huyo mzaliwa wa Msumbiji alitenda kosa hilo Mei, mwaka huu. Fainali za Kombe la Dunia zilianza Juni 11.
Siyo Shirikisho la Soka Ureno (PFF) au Queiroz aliyewahi kuinoa Real Madrid ya Hispania waliozungumza kuhusu adhabu hiyo kama wanakusudia kukata rufani au la. Kocha huyo aliwahi kukaririwa akidai atapinga adhabu hiyo.
Taasisi hiyo ilidai kocha huyo aliingilia majukumu ya uchunguzi wao na mmoja wa madaktari alishindwa kufanya kazi yake kikamilifu ingawa hakuna mchezaji yeyote aliyepatikana na kosa la kutumia dawa za kuongeza nguvu.
Katika utetezi wake, Queiroz alisema alikuwa na hasira baada ya madaktari kuvamia kambi ya Ureno bila taarifa muda ambao nyota wake walikuwa wamepumzika ingawa alikana kutumia lugha isiyofaa.
Kocha msaidizi, Agostinho Oliveira, ataiongoza Ureno katika mechi za kufuzu fainali za Kombe la Ulaya 2012 dhidi ya Cyprus na Norway. Queiroz aliwahi kuwa msaidizi wa Sir Alex Ferguson Manchester United.
No comments:
Post a Comment