LONDON, England
MSHAMBULIAJI nguli wa Manchester United, Michael Owena amemwangukia Sir Alex Ferguson akimtaka ampange katika michezo ya Ligi Kuu England msimu huu.
Owen ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kufunga mabao mawili na kuchangia ushindi wa mabao 5-2 iliyopata United katika mchezo wake wa Kombe la Carling ilipovaana na Scunthorpe.
Mchezaji huyo wa zamani wa England, amerejea katika kiwango bora baada ya kuwa nje ya uwanja muda mrefu kutokana na kukabiliwa na majeraha ya nyonga, amecheza mechi tatu akitokea benchi tangu kuanza msimu huu.
Lakini, Jumatano iliyopita Owen alikuwa nyota wa mchezo baada ya kucheza kwa kiwango bora dakika 90 ingawa Ferguson hakuwepo uwanjani na inadaiwa alikwenda Hispania kuipepeleza Valencia ambayo watakutana nayo wiki ijayo katika mchezo wa ligi ya mabingwa Ulaya.
Baada ya kung'ara katika mchezo huo, mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu za Liverpool, Real Madrid na Newcastle United, ana imani ataonyesha soka ya kuvutia msimu huu baada ya kupona.
"Ilikuwa mechi nzuri kwangu dhidi ya Scunthorpe, nipo katika kipindi cha mpito kwenye michuano ijayo ya ligi ya mabingwa Ulaya na Kombe la Carling. Nina uhakika nitacheza mechi nyingi zaidi," alisema Owen mwenye miaka 30.
Mchezaji huyo anatakiwa kufanya kazi ya ziada kumshawishi Ferguson kumpa nafasi ya kikosi cha kwanza baada ya kocha huyo kuvutiwa na viwango vya Wayne Rooney na Dimitar Berbatov kucheza safu ya ushambuliaji. Berbatov amemshitua Ferguson baada ya Jumapili iliyopita kufunga mabao yote matatu katika mechi dhidi ya mahasimu wao Liverpool.
No comments:
Post a Comment