MFUNGAJI bora wa Ligi Kuu ya Uingereza Didier Drogba ambaye hivi karibuni alitangaza kujitoa kwa muda kuitumikia timu yake ya Taifa ya Ivory Coast ameamua kujiunga tena na timu hiyo baada ya kukutana na Rais Laurent Gbagbo wa nchi hiyo iliyopo Magharibi mwa bara la Afrika mwishoni mwa wiki iliyopita, kwa mujibu wa taarifa ya gazeti moja la michezo nchini humo.
Taarifa ya gazeti hilo iliendelea kusema kuwa Drogba hakuwa na mahusiano mazuri na baadhi ya wachezaji wenzake wa timu hiyo pamoja na viongozi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo . Lakini alihudhuria mchezo ambao timu yake iliirarua Rwanda mabao 3-0 katika kutafuta tiketi ya kucheza michuano ya Mataifa Afrika 2012 kama mshangiliaji.
Rais Gbagbo ni mpenzi mkubwa wa mpira ndio maana akaamua kuingilia kati suala hilo na kumrudisha shujaa huyo wa soka katika timu hiyo baada ya kufanya nae mazungumzo ya kina.
Mshambuliaji huyo wa Chelsea pia alikuna na wachezaji wa timu hiyo kabla ya kuondoka na kurudi katika vilabu vyao na kuwaomba kusahau yaliyopita kwa ajili ya maendeleo ya timu yao ya Taifa, na kuongeza kuwa yuko tayari kuitumikia timu hiyo atapoitwa siku zijazo.
Ivory Coast inatarajiwa kucheza na Burundi Octoba mwaka huu kwa mchezo wa raundi ya pili ya kufuzu michuano ya AFCON.
No comments:
Post a Comment