Tuesday, September 28, 2010

ROONEY KUIKOSA VALENCIA.

LONDON, England
MANCHESTER United imepata pigo baada ya kuripotiwa taarifa kuwa mshambuliaji nguli Wayne Rooney atakosa mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Valencia uliopangwa kuchezwa leo nchini Hispania.

Rooney atalazimika kuangalia mchezo huo akiwa nyumbani na hatakwenda Hispania na kikosi hicho baada ya kuumia kifundo cha mguu katika mchezo walilazimisha sare mabao 2-2 na Bolton kwenye Uwanja wa Reebok.

Nguli huyo wa England, alitoka dakika 61 kupatiwa matibabu ya dharura baada ya kuumia. Mfungaji mabao huyo wa England ameshindwa kurejea katika kiwango chake tangu alipoumia katika mchezo wa ligi ya mabingwa Ulaya msimu uliopita katika mchezo dhidi ya Bayern Munich.

Mshambuliaji huyo alitoka baada ya kupata majeraha lakini kocha Sir Alex Ferguson alisema ana imani Rooney atacheza mchezo huo kwa madai hakupata maumivu makubwa kabla ya jana kuripotiwa taarifa hatacheza pambano hilo kwenye Uwanja wa Mestalla unaotumiwa na Valencia.

"Rooney hatakwenda Hispania wiki hii, meneja amegundua ana maumivu makali hivyo hatakuwa mmoja wa wachezaji watakaocheza dhidi ya Valencia, amepanga kumpumzisha ili kuangalia afya yake," kilisema chanzo cha habari ndani ya klabu hiyo.

Ferguson atalazimika kumtumia mshambuliaji mkongwe, Michael Owen kucheza 'pacha' na Dimitar Berbatov safu ya ushambuliaji. Nyota wamerejea katika viwango bora tangu kuanza msimu huu. Berbatov, alifunga mabao yote matatu katika mchezo ambao United ilishinda mabao 3-2 dhidi ya mahasimu wao Liverpool.

No comments:

Post a Comment