Tuesday, September 28, 2010

VAN GAAL AONGEZA MKATABA BAYERN.

BERLIN, Ujerumani
KOCHA wa Bayern Munich, Louis van Gaal ameongeza mkataba wa mwaka mmoja ambapo mkataba wake sasa utafikia ukingoni Juni 30, 2012.

Kocha huyo raia wa Uholanzi alitia saini mkataba huo juzi Basel, Uswis mji ambao Bayern Munich ilicheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na FC Bassel.

Awali, kulikuwa na taarifa zisizo rasmi kuwa kocha huyo mkongwe, alikuwa kwenye hatihati ya kuongeza mkataba mpya baada ya Bayern Munich kuchapwa mabao 2-1 na Mainz Jumamosi iliyopita.

"Hatuwezi kubadili mwelekeo licha ya kufungwa, tuna imani kubwa na kocha Louis van Gaal. Amefanya kazi kubwa katika timu yetu ni mtu muhimu Bayern Munich," alisema mwenyekiti wa klabu hiyo Karl-Heinz Rummenigge.

Van Gaal mwenye miaka 59, aliipa Bayern Munich ubingwa wa Ligi Kuu Ujerumani mara mbili na Kombe la Ujerumani. Moja ya mafanikio makubwa aliyopata katika rekodi zake ni kuifikisha timu hiyo katika fainali za ligi ya mabingwa Ulaya ambapo timu ilichapwa mabao 2-0 dhidi ya Inter Milan.

No comments:

Post a Comment