UONGOZI wa klabu ya Yanga umesikitishwa na kulaani vurugu zilizosababishwa na mmoja wa viongozi wa wa timu ya Kagera Sugar Mohamed Hussein katika mchezo baina yake na timu hiyo ulichezwa katika Uwanja wa Kaitaba, Kagera ambapo Yanga ilishinda mabao 2-0.
Kauli hiyo imekuja kufuatia Hussein kuonekana akimpiga kwa makusudi Kocha Mkuu wa Yanga Kostadin Papic mara baada ya mpambano wa ligi kuu baina ya timu hizo kumalizika.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Luis Sendeu alisema kitendo kilichofanywa na kiongozi huyo hakikuwa cha kiungwana na kinafaa kulaaniwa na wapenda michezo wote hapa nchini.
Alisema Papic alipigwa wakati akimalizia kuwapongeza wachezaji na waamuzi mara baada ya mchezo huo kumalizika Hussein alipomrushia ngumi kocha huyo na kusababisha vurugu kwa mashabiki walikasirishwa na kitndo hicho.
Alisema uongozi wa klabu hiyo tayari umeliandikia barua Shirikisho la Soka nchini (TFF) juu ya vurugu zilizoanzishwa na kiongozi huyo kwani zingeweza kuleta maafa kwa mashabiki waliohudhuria pambano hilo na kuomba hatua kali za kinidhamu zichukuliwe.
Alisema sio mara ya kwanza kwa Hussein kufanya vurugu katika michezo ya Ligi Kuu kwani aliwahi kufanya vurugu katika miaka ya karibuni katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam hali iliyopekea kutolewa nje na FFU.
"Ni matumaini yetu TFF italichunguza tukio hilo kwa umakini na kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa kiongozi huyo." alimalizia Sendeu.
No comments:
Post a Comment