Wednesday, October 6, 2010

"FERGI ANANITAKA UNITED," - BELLAMY.

LONDON, England
MSHAMBULIAJI mtukutu, Craig Bellamy, amesema kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson alimtupia ndoano kabla ya kutua Cardiff kwa mkopo Agosti, mwaka huu.
 
Mchezaji huyo wa Manchester City, alidokeza Roberto Mancini alimuwekea ngumu kuhamia Old Trafford kutokana na chuki binafsi. Bellay alisema kocha huyo hakupenda kumwona akijiunga na klabu kubwa kabla ya kumsukumia Cardiff kwa mkopo.
 
Nahodha huyo wa Wales, alisema baada ya kutokea mzozo kati yake na Mancini, alitaka kujiunga United baada ya Ferguson kumtaka lakini Mancini aligoma. Bellamy, alisema hakupenda kutua Tottenham Hotspurs kwasababu zilizokuwa nje ya uwezo wake kati ya klabu hizo.
 
"Maisha Manchester City yalikuwa magumu sana, kila kitu kilikuwa kigumu. Manchester United ilinitaka lakini klabu yangu iliweka ngumu na kunisukumia Cardiff haraka sana. Sikuwa na tatizo la kufanya mazoezi mara mbili kwa siku haikuwa tatizo, lakini mzozo wangu na Mancini ulianza baada ya kukosoa baadhi ya mbinu zake" alisema Bellamy.
 
Mkongwe huyo aliibua mzozo na Mancini muda mfupi baada ya kutua Eastaland kuchukuwa nafasi ya Mark Hughes aliyefukuzwa. Nguli huyo alitupiwa virago Liverpool kutokana na tabia ya ukorofi. Bellamy anatajwa mmoja wa washambuliaji wenye vipaji vya kufunga mabao.

No comments:

Post a Comment