Wednesday, October 6, 2010

Mc CLAREN ATAJWA KUMRITHI CAPELLO.

LONDON, England
KOCHA wa zamani wa England, Steve Mc Claren, anatajwa kuwa ndiye mrithi wa Fabio Capello baada ya mkataba wa Mtaliano huyo kumalizika 2012.
 
Capello, ameweka bayana hataongeza mkataba baada ya kumalizika fainali za Kombe la Ulaya 2012.
 
England ilianza vizuri kampeni ya kufuzu fainali hizo kwa kuzichapa Bulgaria mabao 3-1 kabla ya kuifumua Uswis 4-0.
 
Mc Claren alishindwa kuipeleka England katika fainali za Kombe la Ulaya 2008, lakini Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Chama cha Soka England (FA), Trevor Brooking  alisema kocha huyo anastahili kutwaa nafasi ya Capello.
 
"Nina uhakika kama Steve ataendelea kupata mafanikio jina lake litarejea kuinoa England. Tumejifunza mengi, tumepata uzoefu wa kutosha, hatuwezi kumdharau kila mtu nadhani litakuwa siyo jambo zuri," alisema Brooking.
 
McClaren (49), alitupiwa virago England mwaka 2007 lakini nyota yake iling'aa baada ya kutua FC Twente ambapo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu Uholanzi kabla ya kutimkia Ujerumani kujiunga na Wolfsburg miezi mitano iliyopita.
 
Baadhi ya makocha wanaopewa nafasi kuifundisha England ni Harry Redknapp, Sam Allardyce na Roy Hodgson. FA imeweka msimamo kuwa inataka mrithi wa Capello awe raia wa England.

No comments:

Post a Comment