LOME, Togo
RAIS wa muda wa Shirikisho la Soka Togo (TFF), Seyi Memene amejiuzulu kufuatia Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kukataa ombi la bodi ya uchaguzi kutaka kuahirisha uchaguzi kwa wiki mbili.
Waziri wa Michezo wa Togo, Christophe Tchao alisema, Memene aliandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo Septemba 30. Kiongozi huyo wa zamani yupo Paris, Ufaransa alipopelekwa kwa ajili ya kuchunguzwa ugonjwa ambao haufahamiki.
Memene alitaka uchaguzi huo ufanyika Oktoba 16. Shirikisho la Soka Togo, lilikumbwa na kashfa ya kuipeleka timu ya taifa 'feki' kucheza na Bahrain, mkanganyiko huo ulisababisha maofisa wawili Antoine Folly na Doucoure Mamadou kuadhibiwa.
Folly kabla ya kuteuliwa mjumbe wa kamati ya maadili, alikuwa Waziri wa Michezo wa Togo na Mamadou alikuwa msaidizi maalumu wa rais wa Shirikisho hilo. "Nimepokea kopi ya barua ya kujiuzulu kutoka kwa Memene kwasababu anataka kufanyiwa upasuaji mjini Paris," alisema Tchao.
Bodi hiyo sasa imebakiwa na wajumbe sita wa bodi walioteuliwa kwa muda, baada ya jaji Sogoyou Powele na mwanasheria, Akakpo Martial kubwaga manyanga.
Timu ya taifa ya Togo ilipandikizwa majina 'feki' ya wachezaji ilichapwa mabao 3-0 na Bahrain kwenye Uwanja wa Riffa. Shirikisho hilo na Wizara ya Michezo, iliibuka na kudai timu hiyo haikupewa baraka ya kuiwakilisha nchi katika mechi hiyo. Kocha wa zamani wa Togo,Tchanile Bana aliyefungiwa, adhabu yake inaweza kuongezeka.
No comments:
Post a Comment