LONDON, England
SIR Alex Ferguson amewaambia wachezaji wake 'ataua' mtu endapo mwenendo wao utakuwa wa kusuasua katika Ligi Kuu England msimu huu.
Kocha huyo mwenye msimamo, alitoa kauli hiyo juzi usiku akidai haridhishwi na kiwango cha United na ameonya mchezaji yeyote atakayezembea atakiona cha moto.
Ferguson alisema ni upuuzi United kuvuna pointi 13 katika mechi saba ilizocheza na kuwaacha wapinzani wake wakubwa Chelsea kukalia kiti cha uongozi kwa pointi 18.
Alisema hatakubali kuona upuuzi huo ukiendelea na amechukizwa baada ya kikosi hicho kutoka sare mara manne katika mechi saba. "Katika mchezo na Fulham tulikosa penalti kizembe, tulipocheza na Everton walipata mabao mawili dakika za majeruhi, sitakubali upuuzi huu tena," alisema Ferguson.
Kocha huyo alikiri safu ya ulinzi ina tatizo kulinganisha na ushambuliaji na alitaka mabeki kuongeza kasi. Ngome ya United inaundwa na nahodha Gary Neville, Rafael de Silva, Patrice Evra, Nemanja Vidic na Rio Ferdinand aliyekuwa nje ya uwanja muda mrefu akiuguza goti.
Ferguson aliwataka vijana wake kuiga mfano wa Chelsea ambayo ilianza vizuri ligi kwa kupata ushindi mnono mfululizo. Tangu kuanza msimu huu, timu hiyo ya Stamford Bridge imekuwa na kiwango bora.
No comments:
Post a Comment