Tuesday, October 5, 2010

MAN UNITED YAMNYEMELEA LINDEGAARD.

LONDON, England
MANCHESTER United inakaribia kumnasa mrithi wa kipa mkongwe, Edwin van der Sar, Anders Lindegaard baada ya kocha, Eric Steele kumchunguza katika mechi tano alizokaa langoni ikiwemo ya Jumapili iliyopita.
 
Kocha huyo wa makipa, alikwenda Norway kufuatilia kiwango cha Lindegaard wakati timu yake Aalesunds ilipochapwa mabao 2-1 na Stabaeck, lakini mchezaji huyo mwenye miaka 26, alionyesha kiwango bora.
 
Steele pia alikwenda Hispania kuangalia kiwango cha kipa wa Atletico Madrid, David de Gea lakini kocha huyo alionekana kuvutiwa na kiwango cha Lindegaard. United tayari imeanza kumzungumzo na Aalesunds kuangalia uwezekano wa kumsajili kinda huyo anayewindwa na klabu za Liverpool, Arsenal na AC Milan.
 
United inaendelea kufuatilia kiwango cha Lindegaard kabla ya kufikia uamuzi wa kumsajili msimu wa dirisha dogo, Januari, mwakani ili kuchukua mikoba ya mkongwe Van der Sar ambaye mkataba wake unafikia ukingoni mwakani.
 
Mbali ya mchezaji huyo, United inamuwinda beki wa Uruguay, Bruno Montelongo. Mchezaji huyo mwenye miaka 23, anacheza kwa mkopo katika klabu ya AC Milan akitokea River Plate. Timu hiyo imepanga kumtupia ndoano Montelongo ili kusaidiana na Rafael da Silva baada ya nahodha, Gary Neville kustaafu soka mwakani.

No comments:

Post a Comment