LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa Chelsea Didier Drogba amesema kuwa kucheza na timu kama Arsenal ni heshima kubwa kwake, kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja kabla timu hizo kukutana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza Jumapili.
Mchezaji huyo wa kimataifa kutoka Ivory Coast, kama ilivyo kwa wachezaji wengi ambao wameanza kucheza soka ya kulipwa nchini Ufaransa, amekuwa akiifuatilia klabu hiyo toka akiwa mchezaji chipukizi na bado ana mapenzi makubwa kwa klabu hiyo.
"Napenda kucheza mechi kubwa na napenda kucheza dhidi ya Arsenal," Drogba aliiambia luninga ya Sky Sports.
"Siku zote huwa nasema Arsenal ni moja ya timu ninazozipenda.
"Wakati nilipokuwa Ufaransa, Arsenal ilikuwa kama mfano kwetu kwa sababu walikuwa na wachezaji wafaransa ambao walikuwa wakicheza ligi ya huko na wakaondoka kwenda kuichezea Arsenal wakiwa na kocha Mfaransa.
"Kwa hiyo kucheza dhidi yao ina maana kubwa kwangu."
Chelsea inatarajia kurudisha makali yake baada ya kufungwa na Manchester City wiki iliyopita. Drogba anaamini kikosi cha Carlo Ancelotti hakiwezi kupoteza michezo miwili mfululizo.
"Sifikirii kama tutaweza kumudu kupoteza mchezo wa pili, haswa dhidi ya Arsenal," alisema.
"Watu wanatakiwa kujua, na tunajua, kuwa tutapoteza baadhi ya michezo katika msimu huu.
"Lakini narudia, siku zote ni vizuri kushinda."
No comments:
Post a Comment