Tuesday, October 12, 2010

"ULIKUWA NI UAMUZI MGUMU KUIHAMA BARCA." - TOURE YAYA.

LONDON, England
KIUNGO wa Manchester City Yaya Toure ameeleza nia yake ya kurudi katika klabu yake ya zamani ya Barcelona, baada ya kukiri kuwa kuhama Nou Camp "ni jambo gumu katika maisha yangu".

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast alihamia Eastlands katika kipindi cha majira ya kiangazi kwa ada ya euro milioni 24, ambapo klabu hiyo ilikuwa ikimuhitaji kwa kipindi kirefu msimu uliopita".

Toure (27) alisema wakati akihijiwa na Radio Catalunya kuwa atavaa jezi za mabingwa hao wa Hispania tena, akaongeza kuwa ujio wa Sergio Busquets katika kikosi hicho ndio uliochangia maamuzi yake ya kuondoka.

"Nitarudi Barcelona kucheza, sio kama mtalii. Nahitaji kurudi Barcelona, kwasababu kuondoka kwangu kilikuwa ni kitu kigumu katika maisha yangu. alisema Toure.

"Sergio Busquets ni mtu mzuri, na bila Busquets, nisingeweza kuondoka. Ni mchezaji bora na kitu nilichokuwa nahitaji ni kucheza, na sio kukaa benchi. nimeshinda kila kitu nikiwa na klabu ile na nahitaji changamoto tofauti.

"Kwa mimi, Manchester City ni changamoto nzuri. Hii ni timu ambayo haichezi Champions League, na haitawahi kushinda taji lolote hivi karibuni. Kwa hiyo, naona inanifaa."

Barcelona ilimnyakuwa mchezaji huyo kutoka Monaco kwa ada ya euro milioni 9, na ameitumikia klabu hiyo kwa misimu mitatu ya mafanikio ambapo ameshinda mataji mawili ya ligi na moja la Champions League.

No comments:

Post a Comment