SHIRIKISHO la soka nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mechi baina ya timu ya Taifa ya Tanzania "Taifa Stars" na timu ya Taifa ya Morocco mchezo unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage alisema katika mchezo huo kiingilio cha juu kwenye viti vya VIP A kitakuwa sh. 30,000, viti vya VIP B sh. 20,000 na viti vya VIP C sh. 15,000.
Kaijage alivitaja viingilio vingine ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya Bluu, viti vya rangi ya kijani sh. 7,000, wakati viti vya rangi ya machungwa nyuma ya magoli na mkabala na jukwaa kuu sh. 10,000.
Alisema tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zimepangwa kuanza kuuzwa kesho kwenye vituo mbalimbali, Dar es Salaam kuanzia saa 4.30 asubuhi.
"Viingilio hivyo vimepangwa kulingana na mahitaji ya kila mshabiki wa soka, ili aweze kufika uwanjani na kutoa mchango wake kwa kuishangilia Stars ili hatimaye iibuke na ushindi na kuzoa pointi zote tatu," alisema Kaijage.
Wakati huo huo Kaijage alisema Morocco wanatarajiwa kutua leo usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), tayari kwa kuivaa Stars Jumamosi.
Mechi hiyo ya pili kwa Stars ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika, ambazo zimepangwa kuchezwa 2012, zitaandaliwa kwa pamoja na nchi za Gabon na Equatorial Guinea.
Kaijage alisema msafara wa timu hiyo utaundwa na watu 40 ambapo watakuwemo wachezaji, viongozi, makocha wa kikosi hicho pamoja na waandishi wa Habari 15.
"Wageni wetu (Morocco) wanatarajiwa kuwasili kesho usiku (leo), saa 4.30 usiku kwa kutumia ndege za Shirikka la Ndege la KLM. Baada ya kupokewa watapelekwa kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Kempisky," alisema Kaijage.
Kaijage alisema pambano hilo litachezeshwa na waamuzi kutoka Mauritius, ambapo alimtaja mwamuzi wa kati ni Sochurn Rajir ambaye atasaidiwa na waamuzi wasaidizi, Bootun Balkrishna na Vaay Vivian wakati mwamuzi wa akiba Mohammad Imteaz.
Alisema waamuzi hao na kamishna wa mchezo huo, Mohammed Aziz kutoka Kenya, alisema wanatarajia kuwasili nchini kesho usiku.
Kaijage akizungumzia maandalizi ya Stars chini ya kocha wake, Jan Poulsen, alisema maandalizi yanaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na kuwasili kambini kwa wachezaji wote wakiwemo wanaocheza soka ya kulipwa nje ya nchi.
"Idadi yote ya wachezaji 22 wa Stars ambayo imesalia baada ya kuondolewa kikosi Mussa Hassan 'Mgosi', tayari wamesharipoti kambini na wameanza mazoezi. Hivyo tunasubiri tu programu za mwisho za kocha Poulsen kabla ya kuivaa Morocco," alisema.
Mbali ya Morocco na Stars kwenye kundi D, pia ziko timu zingine za taifa za Algeria na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
No comments:
Post a Comment