LONDON, England
KOCHA wa Manchester City Roberto Mancini amesema watakata rufaa dhidi ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa mshambuliaji wao wa pembeni Mario Balotelli walipocheza na West Brom siku ya Jumapili.
Balotelli alioneshwa kadi nyekundu moja kwa moja baada ya kumchezea vibaya Youssuf Mulumbu mchezo ambao City ilishinda mabao 2-0 katika uwanja wa The Hawthorns.
Mancini, anahisi Balotelli hakupaswa kuoneshwa kadi nyekundu, ambayo itamkosesha kucheza mechi Jumatano hii dhidi ya mahasimu wao wakubwa Manchester United.
Mancini alisema: "Sikubaliani kabisa na uamuzi wa mwamuzi kumtoa nje. kadi nyekundu ya nini pale?"
Kocha huyo aliongeza kusema: "Alicheza mchezo mzuri, amefunga mabao mawili, lakini kutolewa kwa kadi nyekundu ni jambo lisiloeleweka.
"Nataka kufahamu kwa nini ilikuwa ni kadi ya moja kwa moja nyekundu. Nionavyo haikuwa sahihi na mwamuzi ni lazima atoe maelezo.
"Nimekasirika kwa sababu nilizungumza naye kabla ya mechi, awe makini na mwamuzi. Nilikuwa nataka kumuingiza Adam Johnson badala yake, lakini sikuwa na muda wa kufanya mabadiliko hayo." Aliongeza Mancini.
Ushindi huo muhimu wa Man City umekuja baada ya timu hiyo kupokea vipigo vitatu mfululizo, na umeinua matumaini ya kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao wakijizatiti nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu ya England.
Manchester City katika mchezo huo walikuwa na nahodha wao aliyekuwa majeruhi Carlos Tevez.
No comments:
Post a Comment