LONDON, England
KOCHA wa Chelsea, Carlo Ancelotti, amesema hana mpango wa kumnunua mshambuliaji nyota wa Liverpool, Fernando Torres katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani.
Kauli ya Mtaliano huyo imekuja muda mfupi baada ya Torres kufunga mabao yote mawili katika mchezo wa ligi dhidi ya Chelsea uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Anfield. Katika mchezo huo Liverpool ilishinda mabao 2-0.
Ancelotti alisema hana mpango wa kumnyakuwa nyota huyo kwa madai anaye mshambuliaji mwenye kiwango bora, Didied Drogba na kuongeza kuwa nahodha huyo wa Ivory Coast ana nafasi ya kung'ara katika kikosi chake kutoka makao makuu Stamford Bridge.
Kocha huyo ametoa ufafanuzi huo baada ya kuibuka tetesi ana mpango wa kutoa pauni milioni 50 (sh. bilioni 115) kumsajili msimu wa dirisha dogo. "Taarifa hizi ni kama zile zilizovuma za Carlos Tevez, sina mpango wa kumsajili Torres, tuna washambuliaji imara wenye uwezo wa kufunga mabao," alisema Ancelotti.
Ancelotti alidokeza kuwa anapokuwa na Drogba (32) na Nicolas Anelka, hana hofu ya kuongeza mchezaji yeyote wa safu yake ya ushambuliaji kwa kuwa nyota hao wapo fiti. Kocha huyo alisema licha ya kufungwa na Liverpool, ana amini ubingwa upo mikononi mwao na ameahidi kufanya vizuri mechi zijazo.
Kocha huyo amekuwa akiwatumia washambuliaji Drogba na Anelka kucheza 'pacha' safu ya ushambuliaji akiwemo nyota mwingine wa Ufaransa, Florent Malouda anayecheza pembeni mwa uwanja. Chelsea ndio mabingwa watetezi wa ligi kuu England.
No comments:
Post a Comment