LONDON, England
HARRY Redknapp amemshambulia vikali mwamuzi maarufu, Howard Webb na mashabiki wa klabu ya Tottenham Hotspurs muda mfupi baada ya timu hiyo kulazimisha sare bao 1-1 na Sunderland katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa juzi usiku.
Kocha huyo alifura kwa hasira baada ya Webb aliyecheza mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia kati ya Hispania na Uholanzi baada ya kumwonyesha kadi ya njano mshambuliaji, David Bentley kwa madai ya kujirusha ndani ya eneo la hatari kutafuta penalti.
Katika mchezo huo, mshambuliaji nyota wa Ghana aliyeng'ara katika fainali za Kombe la Dunia, Asamoah Gyan aliiokoa Sunderland baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika 67. Tottenham iliyokuwa nyumbani ilitangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa Van der Vaart dakika 64.
Bentley alijiangusha ndani ya eneo la hatari akiwa amezongwa na Bolo Zenden. Mbali ya kumbwatukia Webb, Redknapp aliwashukia baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo waliojawa hasira kwa kutoridhishwa na matokeo hayo.
"Ilikuwa ni penalti ya dhahiri niliangalia marudio ya mchezo ule, kwanini alimpa kadi? Mwamuzi hakuwa makini na kazi yake kwa sababu ilikuwa ni penalti ya wazi, nadhani hakufanya kazi yake ipasavyo. Endapo tungepata ingetusaidia kupunguza tofauti kubwa ya idadi ya pointi," alisema Redknapp.
No comments:
Post a Comment