LONDON, England
RUFANI iliyokatwa na klabu ya Manchester City kupinga adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa mshambuliaji wake nyota, Mario Balotelli imegonga mwamba kwa Chama cha Soka England (FA).
Balotelli aliyejiunga Man City majira ya kiangazi akitokea Inter Milan, alifunga mabao mawili katika mchezo wa ligi dhidi ya West Bromwich uliochezwa Jumapili iliyopita kabla ya kulimwa kadi nyekundu. Man City ilishinda mabao 2-0.
Kocha wa Man City, Roberto Mancini, alipeleka malalamiko FA kupinga kadi hiyo, lakini Chama hicho kimetupilia mbali rufani hiyo na mchezaji huyo ataendelea kutumikia adhabu ya kukosa tatu mbili. Mwamuzi, Lee Probert, alimtoa nje Balotelli (20) alimchezea rafu beki, Youssouf Mulumbu.
Mshambuliaji huyo mtukutu alianza kutumikia adhabu hiyo kwa kukosa mechi ngumu kati yao na mahasimu wao Manchester United na atakuwa jukwaani katika michezo miwili dhidi ya Birmingham na Fulham.
Katika hatua nyingine, kiungo mwenye sifa ya kucheza rafu mbaya, Nigel de Jong amemtaka Balotelli kujichunga kuepuka adhabu kutoka kwa waamuzi. Muda mfupi baada ya kuanza kazi Man City, Balotelli aliwahi kusema ligi ya England ni ngumu kwa madai wachezaji wake wanacheza rafu zaidi kulinganisha na Italia.
No comments:
Post a Comment